Waandamanaji nchini Myanmar wamekabiliana na vikosi vya usalama hii leo huku umoja watawa wa Kibuddha wakitoa mwito kwa utawala wa kijeshi kusitisha matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji.
Matangazo
Waandamanaji nchini Myanmar wamekabiliana na vikosi vya usalama hii leo huku umoja wa watawa wa Kibuddha wakitoa mwito kwa utawala wa kijeshi kusitisha matumizi ya nguvudhidi ya waandamanaji na kulituhumu kundi hilo la wachache lililojihami kwa silaha kwa kuwatesa na kuwauwa raia wasio na hatia tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita.
Waandamanaji hao walitumia manati kukabiliana na polisi na wengine aliwatupia mabomu ya kutengeneza kwenye chupa za vilevi, katika tukio ambalo ni la nadra la kupambana dhidi ya vikosi vya usalama vinavyokabiliana vikali na waandamanaji hao wanaoyapinga mapinduzi.
Kuongezeka kwa makabiliano hayo kunafuatia tamko la shirika moja kwamba zaidi ya watu 200 wameuawa tangu Februari Mosi. Takriban watu wawili waliuawa wakati wa maandamano hii leo katika eneo la kaskazinimagharibi mwa Myanmar, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari na machapisho ya kwenye mitandao ya kijamii yaliyoonyesha picha za wahanga.
Katika kile kinachoonekana kama ukosoaji wa wazi kabisa dhidi ya hatua kali na za ukandamizaji zinazochukuliwa na wanajeshi dhidi ya waandamanaji, kamati ya watawa hao iliyoteuliwa na kiserikali ya Sangha Maha Nayaka pia imesema kwenye muswada wa taarifa yake kwamba inakusudia kusimamisha shughuli zake, kama hatua moja wapo ya kuupinga utawala huo.
Inapanga kuchapisha rasmi taarifa hiyo baada ya kuwasiliana kwa waziri anayeshughulikia masuala ya dini kesho Alhamisi.
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis hii leo ametoa mwito wa kumalizwa kwa machafuko ya umwagaji damu nchini humo. Papa Francis amerejea picha zilizowaonyesha watawa wa kanisa hilo nchini Myanmar wakiwa wamepiga magoti barabarani mbele ya wanajeshi wa usalama, na kusema hata yeye anapiga magoti kwenye mitaa ya Myanmar na kuomba machafuko hayo kusitishwa.
Amesema "Kwa mara nyingine na kwa huzuni kubwa, ninatamani kuzungumza juu ya hali ya kushangaza huko Myanmar, ambapo watu wengi, haswa vijana, wanapoteza maisha yao ili kuleta matumaini kwenye nchi yao. Mimi pia napiga magoti kwenye mitaa ya Myanmar, nami nasema, Acheni vurugu. Umwagaji damu hausuluhishi chochote, mazungumzo yanaweza kuleta suluhu."
Myanmar: Waandamanaji wapigwa kwa mabomu ya machozi na vifaa vya kupiga shoti ya umeme
Waandamanaji walikabiliwa na vikosi vya usalama, baada ya siku mbaya zaidi tangu mapinduzi ya mwezi uliopita.
Picha: AFP/Getty Images
Maandamano barabarani
Mwandamanaji aliyevaa kifaa cha kuzuia gesi ameketi kwenye barabara iliyofungwa huko Yangon. Polisi huko Yangon walifyatua gesi ya kutoa machozi dhidi ya umati wa watu ambao walirudi barabarani kupinga mapinduzi ya mwezi uliopita.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Sura ya Suu Kyi ipo daima
Waandamanaji waliovalia kofia ngumu za usalama wanapiga kelele na kuonyesha picha za kiongozi wa Myanmar aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi wakati wa maandamano ya kupinga mapinduzi nyuma ya kizuizi kwenye barabara iliyofungwa huko Yangon. Waandamanaji waliingia barabarani wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Kusini Mashariki mwa Asia wakijiandaa kukutana kuujadili mgogoro huo.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Mabomu ya kutoa machozi huko Mandalay
Eneo hili, kutoka Jumanne, linaonyesha waandamanaji wakiondoka kwenye wingu la gesi ya kutoa machozi huko Mandalay. Waandamanaji kote nchini walivaa kofia ngumu na ngao za kutengeneza, na kukusanyika nyuma ya vizuizi wakati wakiimba na kupiga saluti kwa kutumia vidole vitatu.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Saluti ya vidole vitatu kwa ajili ya demokrasia
Saluti hii ya vidole vitatu imekuwa ishara ya maandamano huko Myanmar. Awali ilionyeshwa katika vitabu vya "Hunger Games" na vipindi vya runinga na mara ya kwanza ilifanywa na wafanyikazi wa matibabu wanaopinga mapinduzi. Hakukuwa na ripoti za majeraha yoyote huko Yangon Jumanne, lakini walioshuhudia walidai kwamba watu kadhaa walijeruhiwa magharibi mwa mji wa Kale.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Machafuko katika mitaa
Waandamanaji wanaangalia mwendo wa lori la polisi wakati wa maandamano ya kupinga mapinduzi kwenye barabara iliyofungwa huko Mandalay Jumanne, Machi 2. Waandamanaji pia waliandamana kupitia mitaa ya Dawei, mji mdogo kusini mashariki mwa Myanmar ambao umekuwa na maandamano karibu kila siku dhidi ya utawala wa jeshi.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Kuomboleza waliokufa
Watu wanasali karibu na jeneza la mwanamke ambaye familia yake ilisema aliuawa na jeshi Jumapili, wakati wa ibada yake ya mazishi huko Mandalay Jumatatu, Machi 1. Kulingana na Umoja wa Mataifa takriban watu 18 waliuawa na vikosi vya usalama Jumapili.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Waandamanaji dhidi ya polisi
Mwandamanaji amtupia sehemu ya ndizi polisi wakati wa maandamano huko Yangon Jumanne, Machi 2. Mamia walikusanyika katika eneo la Hledan la Yangon, ambapo siku iliyopita polisi walikuwa wametumia mabomu ya kutoa machozi mara kadhaa.
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance
Waandamanaji wanawaomboleza wahanga wa mwishoni mwa wiki
Mwombolezaji anahudhuria mazishi ya Jumanne ya Nyi Nyi Aung Htet Naing, ambaye alikufa kutokana na jeraha la risasi wakati akihudhuria maandamano huko Yangon. Waandamanaji wameendelea kuingia mitaani kote Myanmar licha ya kushuhudia mwishoni mwa wiki iliyopita iliyomwaga damu zaidi tangu mapinduzi ya Februari.
Picha: AFP/Getty Images
Picha 81 | 8
Maandamano dhidi ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa serikali iliyochaguliwa ya Aung San Suu Kyi kwa muda mrefu yalikuwa ya amani lakini hii leo baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji wa mji mkuu wa Yangon, walitawanyika na baada ya muda walirudi wakiwa na kuweka vizuizi vya mifuko vya michanga. Baadhi yao walirusha mabomu ya kutengeneza kwenye chupa za vilevi na wengine walitumia manati kuwalenga wanajeshi, ingawa haikuwa rahisi kuwafikia.