1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Myanmar kupinga mapinduzi ya jeshi

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
6 Februari 2021

Maandamano makubwa yameshuhudiwa nchini Myanmar. Kundi kubwa la vijana limeingia barabarani kuupinga utawala mpya wa jeshi la nchi hiyo, licha ya kuzimwa kwa mitandao kote nchini kwa lengo la kuudhoofisha upinzani.

Myanmar Rangun | Proteste nach Militärputsch
Picha: STR/AFP/Getty Images

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kwenye Twitter kwamba huduma za mitandao na mawasiliano lazima zirejeshwe kikamilifu kuhakikisha uhuru wa kujieleza na wa kupata habari. Mkuu wa sera ya umma ya mtandao wa Facebook kwa eneo la Asia-Pacific Rafael Frankel amesema kwenye taarifa yake kwamba katika wakati huu muhimu, watu wa Myanmar wanahitaji kupata habari na kuweza kuwasiliana na familia zao.

Soma Zaidi:Aung San Suu Kyi afunguliwa mashtaka baada ya mapinduzi

Hata hivyo kuzimwa kwa mitandao hakukuwazuia maelfu ya waandamanaji hao kukusanyika katika jiji kuu la Myanmar, Yangon mnamo siku ya Jumamosi. Mikusanyiko ilianzia kwenye barabara iliyo karibu na Chuo Kikuu cha Yangon ambapo waandamanaji walipunga mikono kwa ishara ya vidole vitatu vya kati ambayo imekua ndio ishara ya kupinga uporaji wa madaraka uliofanywa na jeshi.

Kikosi kikubwa cha polisi wa kuzuia ghasia kilifunga barabara za karibu na maeno walipokusanyika waandamanji, na malori mawili ya maji ya kuwasha yakiwa yameegeshwa katika eneo hilo.

Kiongozi wa chama cha NLD Aung San Suu KyiPicha: Taro Nishijima/Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Miito ya kupinga mapinduzi ya jeshi iliyotolewa mitandaoni kabla ya kufungwa imepokelewa kwa kishindo na wanapinga waziwazi hatua iliyochukuliwa na jeshi. Uasi huo wa wananchi wa Myanmar ni pamoja watu kote nchini kupiga makelele kwa kuyagonga masufuria zoezi ambalo kwa kawaida linahusishwa na shughuli za kitamaduni za kuyafukuza mapepo na mambo mengine maovu.

Kwingineko makundi mengine mawili ya waandamanaji yalikusanyika katika mji wa Sule Pagoda ulio kusini mwa jiji la Yangon, waandamanaji hao walibeba mabango yenye maandishi na picha za kiongozi wao San Suu Kyi na rais Win Myint wakitaka waachiliwe. Waandamanaji hao wamesema watarudi tena mitaani Jumapili.

Shirika la habari la AFP limeripoti juu ya maandamano mengine katika mji wa Kaskazini wa Mandalay, ambako watu wapatao elfu mbili pia waliandamana.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar  amefanya mawasiliano ya kwanza na naibu kamanda wa jeshi la Myanmar ambapo amelihimiza jeshi kurudisha madaraka mikononi mwa serikali ya kiraia.

Wahudumu wa afya wa hospitali kuu ya Yangon waunga mkono maandamano ya kupinga jeshi kutwaa madaraka.Picha: REUTERS

Vyombo vya habari vya serikali nchini Myanmar viliripoti Jumamosi kwamba maafisa walizungumza na wanadiplomasia mnamo siku ya Ijumaa ili kujibu matamko yaliyotolewa na jumuiya ya kimataifa.

Rais wa Marekani Joe Biden alikuwa miongoni mwa viongozi wa ulimwengu wiki hii kuwataka majenerali waachie madaraka waliyoyatwaa kimabavu, wawaachilie mawakili, wanaharakati, maafisa waliowashikilia pamoja na kuondoa vizuizi katika mawasiliano ya simu. Rais Biden pia aliwataka majenerali hao waepuke vurugu.

Wabunge waliochaguliwa

Mnamo siku ya Ijumaa, takriban wabunge 300 waliochaguliwa kutoka wa chama cha NLD cha Aung San Suu Kyi walikutana kwa njia ya mtandao na kwenye mkutano huo walitangaza kuwa wao ndio wawakilishi halali wa watu wa Myanmar na walihimiza kutambuliwa kimataifa kama serikali ya nchi hiyo.

Walipaswa siku ya Jumatatu kuhudhuria kikao ukiwa mwanzo wa muhula mpya bungeni baada ya kufanyika uchaguzi mwezi Novemba ndipo jeshi lilipotangaza kuwa limetwaa madaraka kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Jeshi limemlaumu Aung San Suu Kyi na chama chake cha NLD kwa kushindwa kuchukua hatua baada ya malalamiko kwamba uchaguzi huo wa Novemba uligubikwa na ulaghai, ingawa tume ya uchaguzi imesema haijapokea ushahidi wowote kuunga mkono madai hayo. Suu Kyi na Rais Win Myint bado wamezuiwa nyumbani na wameshtakiwa kwa makosa madogo madogo ambayo wengi wanayaona ni kama sababu tu ya kuhalalisha kuzuiwa kwao.

Vyanzo:/AFP/AP