Myanmar: Serikali yazingatia kura ya maoni zaidi ya maafa ya Nargis
9 Mei 2008Myanmar imekubali misaada ya kimataifa lakini imesema haitoruhusu wafanyikazi wa misaada.
Serikali hiyo imesema hayo baada ya kuirejesha nyumbani ndege iliyokuwa na waokoaji kutoka Qatar.
Wakati huo huo serikali ya kijeshi ya Myanmar imetoa wito kwa wananchi wake kupitisha katiba ya utawala wa kijeshi katika kura ya maoni hapo kesho.
Taarifa hizo za kukataa wafanyikazi wa misaada na kukubali misaada zimechapishwa leo na wizara ya nchi za nje katika gazeti la serikali la Myanma Ahlin.
Ndege ya Qatar ilikuwa 1 kati ya ndege 12 za kimataifa zilizotua mjini Yangun hapo jana.
Shutuma zimeendelea kutolewa kwa serikali hiyo ya kijeshi kufuatia jinsi inavyoshughulikia janga lililosababishwa na kimbunga cha Nargis. Vile vile jamii ya kimataifa imegadhabishwa na jinsi serikali hiyo inavyochelewesha vibali vya visa kwa wafanyikazi wa kimataifa na idhini ya kutua kwa ndege za misaada.
Balozi wa Marekani nchini Tailand Eric John anasema watu wanaendelea kuteseka. "Kila siku visa hizi zinapocheleweshwa watu wengi zaidi wanateseka Burma na tunataka kusaidia na tunaitaji visa ili kusaidia"
Umoja wa Mataifa unasema hatua hiyo ya kuwakataa wafanyikazi wa misaada wakati kama huu haijawahi kushuhudiwa katika historia ya kusaidiana kimataifa.
Takriban wiki moja imepita tangu kimbunga cha Nargis kilipovuma kwa kasi ya kilomita 190 kwa saa na kuvunja kingo za bahari ambayo baadaye ilifurika katika maeneo ya chini ya Irrawaddy delta. Manusura wengi bado hawajafikiwa na misaada.
Vijiji vilifinikwa na maji na miili ya watu wengi ikabakia ikiolea katika shamba la mchele la delta ambalo kwa wakati mmoja lilikuwa likizalisha mchele unaolisha bara zima la Asia.
Waziri wa ulinzi nchini Marekani Robert Gates anasema nchi hiyo iko tayari kutoa msaada wake. "Kuna nafasi ya kuokoa maisha ya watu wengi na tuko tayari kabisa kufanya hivyo mara moja. Na itakuwa jambo la kuhuzunisha iwapo watu hawatakuikubali fursa hii"
Idadi kamili ya waliouwawa na kimbunga cha Nargis ingali inasemekana kuwa takriban watu 23,000 na wengine 42, 119 hawajulikani walipo. Hata hivyo wataalamu wanasema huenda idadi hiyo imefika watu 100,000.
Wakati maji ya chumvi yanachanganyikana na maji ya visima, magala ya nafaka na mashamba ya mchele watu wengi huenda wakakumbwa na magonjwa yatakayosababisha vifo zaidi.
Kulingana na Umoja wa Mataifa watu takriban 1.5 kati ya wamianmar milioni 53 wameathirika na na wanahitaji vyakula na makaazi.
Lakini wakati hayo yanajiri serikali ya mianmar imetoa wito kwa wananchi wake kushiriki katika kura ya maoni itakayofanyika kesho na kuichagua katiba iliyotayarishwa na jeshi.
Wito huo uliotolewa kupitia televisheni haukugusia chochote kuhusu mamilioni ya watu walioathirika na kimbunga cha Nargis ambao hawatashiriki katika kura hiyo kwani imehairishwa katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Wapinzani nchini humo wanasema sababu ya serikali hiyo kukataa wafanyikazi wengi wa kimataifa ni kuona kwamba kura ya maoni ya kesho inafanyika kwanza kabla ya kuwaruhusu wafanyikazi hao waingie.
Kura hiyo ya maoni inafanyika kesho katika maeneo mengi mianmar na baada ya wiki mbili itafanyika tena katika maeneo ya kusini yaliyoharibiwa na kimbunga cha Nargis.
Mara ya mwisho uchaguzi kufanyika nchini humo mwaka wa 1991 chama cha National League for Democracy kinachoongozwa na Aung San Suu kiliishinda serikali kwa kura nyingi.
Waziri mkuu wa Tailand Samak Sundaravej ambaye alikuwa anatarajiwa kusafiri hadi Mianmar mwishoni mwa wiki amekatiza safari hiyo akisema hakuna haja ya ziara hiyo kufanyika wakati wafanyikazi wa misaada wa kimataifa hawaruhusiwi kuingia nchini humo.
Hata hivyo meli ya pili kutoka China yenye tani 60 za misaada ya madawa, mahema, vyakula, maji na vifaa vingine vya misaada imewasili leo nchini humo.