Myanmar wafanya uchaguzi
8 Novemba 2015Katika kukumbusha nyota ya nguvu za Suu Kyi , kiongozi huyo wa upinzani, akivalia nguo yake ya kimila ikirembeshwa kwa shada la maua kichwani , alizingirwa na waungaji wake mkono katika kituo cha kupigia kura , wakiimba "ushindi , ushindi" wakati mwanamke huyo shujaa wa taifa akipita katikati ya kundi la watu.
Chama chake cha National League for Democracy (NLD) kinaamini uchaguzi wa haki utakiingiza madarakani baada ya mapambano ya miongo kadhaa dhidi ya udikteta wa jeshi la nchi hiyo.
Lakini mshindi huyo wa nishani ya amani ya Nobel anazuiwa kuwania urais na katiba iliyoandikwa na jeshi na chama cha NLD kinakabiliwa na kibarua kigumu wakati robo ya viti bungeni vimetengwa kwa ajili ya jeshi.
Akifahamika na wafuasi wake kwa jina la "mama Suu", anajitokeza juu kabisa ya vuguvugu la kudai demokrasia nchini humo, akiwa kama nguvu inayoendesha chama cha NLD.
"Nimepiga kura yangu, kazi yangu imemalizika," amesema Myint Aung mwenye umri wa miaka 74, katika kituo cha kupigia kura cha mjini Yangon ambako Suu Kyi alipiga kura.
"Nimepiga kura kwa mtu ambaye watu wanamtaka atawale," amesema kwa bashasha, kabla ya kuonesha kidole chake cha mwisho alichokichovywa katika wino wa rangi ya zambarau kuonesha kwamba amekwisha piga kura.
Hamasa ya kupiga kura
Misururu ya watu , wengi wakivalia nguo za kitamaduni za saruni Longyi , imejitokeza mapema kabla ya alfajiri katika vituo vya kupigia kura nchini humo katika ishara ya hamasa ambayo inakwenda sambamba na uchaguzi huo wa kihistoria, unaowekewa matumaini kwamba ni uchaguzi wa haki kabisa kwa kizazi hiki.
Taifa hilo la kusini mashariki mwa bara Asia limetawaliwa kwa miongo mitano na utawala katili wa kijeshi ambao umekandamiza upinzani kwa nguvu na kuwaweka jela.
Lakini katika mwaka 2011 utawala huo wa kijeshi ghafla ulikabidhi madaraka kwa serikali iliyokuwa na mchanganyiko wa wanajeshi na raia ikiongozwa na jenerali wa zamani wa jeshi.
Mageuzi yaleta unafuu
Mageuzi ya haraka tangu wakati huo yameleta afueni katika uchumi wa nchi hiyo uliokabwa na kuleta mageuzi mengi kwa watu wa nchi hiyo , waliotengwa na kuchoshwa--ikiwa ni pamoja na kuachiwa huru kwa wafungwa wengi wa kisiasa.
Kiasi ya watu milioni 30 wana haki ya kupiga kura, katika tukio ambalo limesababisha changamoto nyingi za usafirishaji katika taifa hilo kubwa na masikini.
Wapiga kura wengi wanabaki kuwa na wasi wasi kuhusiana na vipi jeshi lenye nguvu nyingi litachukua hatua iwapo litashindwa.
Udanganyifu umetokea mara nyingi katika chaguzi zilizopita, lakini maafisa wa tume ya uchaguzi wanasisitiza upigaji kura umeanza vizuri na unakwenda vizuri hadi sasa.
Vituo vya uchaguzi vitafungwa jioni na shauku itageukia katika makao makuu ya chama cha NLD mjini Yangon ambako televisheni kubwa zitakuwa zinaonesha hesabu ya kura wakati matokeo yatakapokuwa yanaanza kuingia kutoka maeneo mbali mbali ya nchi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Isaac Gamba