Myanmar yaadhimisha miaka 75 ya uhuru wake
4 Januari 2023Kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Jenerali Min Aung Hlaing, amedokeza leo juu ya mipango ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu baadae mwaka huu na kutaka mshikamano wa kitaifa katika hotuba yake wakati alipoongoza hafla ya maadhimisho ya miaka 75 ya uhuru wa taifa hilo kutoka Uingereza.UN yapitisha azimio la kumalizwa kwa machafuko Myanmar
Kiongozi huyo amezitolea mwito nchi nyingine na mashirika ya kimataifa pamoja na watu wa Myanmar kuunga mkono "mfumo wa kweli wa demokrasia ya vyama vingi unaostawi kwa nidhamu" ambao jeshi tawala linautaja kuwa lengo lake.
"Tumekabiliwa na ukosoaji, shinikizo na mashambulizi kutoka kwa mashirika ya kigeni dhidi ya uamuzi wetu. Na ninataka kusema asante kwa baadhi ya nchi za kimataifa na kikanda, mashirika na watu binafsi ambao wanaelewa hali yetu ya sasa katika siasa na wanashirikiana nasi vyema."
Hatua ya kwanza kuelekea kuitisha uchaguzi mkuu inaweza kutokea mwishoni mwa mwezi huu, wakati ambapo muda wa sasa wa miezi sita wa hali ya dharura utakuwa ukimalizika. Hali hiyo ilitangazwa kuruhusu utawala wa kijeshi baada ya jeshi kunyakua madaraka mnamo Februari mwaka 2021 kutoka kwa serikali ya kiraia ya Aung San Suu Kyi.
Taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia, limekabiliwa na mbinyo wa kimataifa pamoja na vikwazo vya mataifa ya magharibi tangu jeshi lilipochukua madaraka. Myanmar ilitumbukia katika ghasia tangu mapinduzi hayo yaliyosababisha kukamatwa kwa Suu Kyi na maafisa wengine wa chama chake. Jeshi limekabiliana na waandamanaji wanaounga mkono demokrasia pamoja na wapinzani kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Hivi karibuni Suu Kyi alitiwa tena hatiani kwa makosa matano yanayohusiana na rushwa na kufungwa miaka saba zaidina kukamilisha mkururo wa mashitaka ambayo yamekosolewa kimataifa kama njama za utawala wa kijeshi kuendeleza kitisho chake katikati mwa upinzani mkubwa wa ndani dhidi ya utawala huo.
Ingawa chama cha Suu Kyi cha National League for Democracy hakijafutwa, lakini kwa kiasi kikubwa kimedhoofika kisiasa kutokana na viongozi wake na wanachama wengi kuishia jela au kukimbilia mafichoni.
Myanmar ilitangaza uhuru wake kutoka Uingereza mnamo Januari 4 mwaka 1948 baada ya harakati za ukombozi za muda mrefu ambazo ziliongozwa na Jenerali Aung San ambaye ni baba wa kiongozi wa kiraia aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi.