1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

Myanmar imeingia mwaka wa 4 baada ya mzozo wa mapinduzi

Hawa Bihoga
1 Februari 2024

Myanmar leo inaingia mwaka wake wa nne tangu kufanyika kwa mapinduzi yaliomaliza utawala wa kidemokrasia, huku utawala wa kijeshi ukionya kuwa "utafanya lolote" kuwaminya wapinzani katika utawala wake.

Naypyitaw, Myanmar | Mkuu wa Jeshi Min Aung Hlaing
Mkuu wa Jeshi Myanmar Min Aung Hlaing akihutubia taifaPicha: Myawaddy/AP Photo/picture alliance

Utawala wa kijeshi wa Myanmar uliongeza muda wa sheria ya hali ya dharura kwa miezi sita kabla ya kumbukumbu hiyo ya mapinduzi, huku kwa mara nyingine wakichelewesha tena uchaguzi ulioahidiwa, na kuendelea kukandamiza upinzani unaokuwa katika utawala huo.

Mitaa katika mji mkuu wa Yangon ilikuwa ni tulivu majira ya asubuhi ya leo Alhamisi kuliko kawaida, kutokana na wapinzani kuwatolewa mwito wakaazi kusalia majumbani ikiwa ni kile kilichotajwa kuwa ni "mgomo baridi" dhidi ya mapinduzi hayo.

Usafiri wa umma katika majira ya asubuhi mara zote unakuwa umejaza, lakini siku ya leo umeshuhudiwa ukiwa tupu.

Soma pia:Myanmar yaingia mwaka wa 4 baada ya mapinduzi

Katika moja ya soko la wachuuzi ambalo huwa na shughuli nyingi, wafanyabiashara wameonekana wakifunga maduka yao.

"Sitatoka nje kati ya saa 10 asubuhi na saa kumi jioni leo," mfanyakazi mmoja katika mji wa Yangon alisema, akirejelea nyakati za "mgomo baridi."

"Nimeridhika kuona hakuna watu wengi mitaani,"  alisema raia mmoja ambae hakutaka kutaka jina lake lifahamike kutokana na sababui za kiusalama.

"Hii ni alama ya umoja wetu, dhidi ya mapinduzi." Aliongeza.

Maandamano ambayo yamewakusanya mamia ya waandamanaji yameshuhudiwa pia nchini Thailand, wakipinga utawala wa kijeshi wa Myanmar.

Moja ya mtaa wenye shughuli nyingi katika mji wa Yangoni ukiwa tupu katika kile kinachotajwa "mgomo baridi."Picha: AFP/Getty Images

Vijana, wazee walikusanyika nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Bangkok, nchini Thailand wakiwa wamevalia fulana zinazomuonyesha kiongozi wa demokrasia aliyefungwa jela Aung San Suu Kyi, wakiwa na maua meupe kwenye nywele zao na vitambaa vyekundu kwenye paji la uso.

Kumbukumbu hii inafanyika wakati taifa hilo la Asia linakabiliwa na changamoto ya usalama, vikwazo vya kikanda na hata kimataifa.

Juhudi za kimataifa kurejesha utawala wa kiraia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo Alhamisi ametolea mwito wa kukomesha ghasia na kurejea katika demokrasia katika kumbukumbu hii, wakati siku ya Jumatano Marekani ilitangaza awamu mpya ya vikwazo dhidi ya utawala wa kijeshi.

Katika taarifa ya katibu Mkuu Guterres kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, alihimiza udharura wa kuundwa kwa njia ya kuelekea utawala wa mpito wa kidemokrasia na kurejesha utawala kamili wa kiraia.

Juhudi za kidiplomasia za kumaliza mzozo zikioongozwa na Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia ASEAN hazijafanikiwa.

Viongozi wa ASEAN wakiwa katika picha ya pamojaPicha: Indonesian Presidential Secretariat Press Bureau

Soma pia:Makundi ya makabilia yaliyojihami kwa silaha nchini Myanmar yauteka mji wa Namhsan

Jana Jumatano katika taarifa yao ya pamoja mawaziri wa mambo ya nje wa Australia, Canada, New Zealand, Norway, Korea Kusini, Uswisi, Uingereza na Marekani, na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, walitoa wito kwa jeshi kuwaachilia wafungwa wa kisiasa na kusitisha ghasia dhidi ya raia.

Mapema Februari 1, 2021, vikosi vya usalama vilimkamata mshindi wa Tuzo ya Nobel Aung San Suu Kyi na wabunge wa chama chake cha National League for Democracy NLD, walipokuwa wakijiandaa kuingia bungeni.

Jeshi lilidai kuwa udanganyifu mkubwa ulifanyika wakati wa uchaguzi wiki zilizopita, wakati NLD ilipomshinda mpinzani anayeungwa mkono na jeshi.

Hata hivyo, waangalizi wa uchaguzi huo  walihitimisha kuwa kwa kiasi kikubwa ulikuwa huru na wa haki.

Hatua hiyo ilizusha maandamano makubwa kwa nchi nzima yakipinga mapinduzi hayo, lakini yalikabiliwa na ukandamizaji wa kikatili na endelevu ambao ulisababisha maelfu ya waandamanaji kutafuta njia za kujitetea.

Soma pia:Canada, Uingereza na nchi kuu za EU zajiunga na kesi ya mauaji ya halaiki Myanmar

Kufuatia kadhia hiyo ambayo ilivuta nadhari ya kikanda na kimataifa, zaidi ya watu 4,400 waliuawa katika harakati za kijeshi dhidi ya wapinzani na zaidi ya 25,000 kukamatwa, ikiwa ni kwa mujibu ya wafuatiliaji wa masuala ya ndani ya Myanmar.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mapigano na kulipiza kisasi yameharibu maeneo mengi ya Myanmar na kuwalazimu zaidi ya watu milioni mbili kukimbia makazi yao.

Hali ya haki za binadamu chini ya utawala wa kijeshi

Mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ndani ya juma hili alisema kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Myanmar inazidi "kuzorota."

Alisema watawala wa kijeshi wamewatesa wanavijiji, wametekeleza mauaji ya kiholela na walifanya mashambulizi ya anga na kuvurumisha mabomu pamoja na kuwapiga risasi, kuwaadhimu wapinzani wa utawala huo na makundi ya watetezi wa haki za binadamu.

UN: Mauaji bado yanaendelea Myanmar

01:06

This browser does not support the video element.

Aidha utawala huo umeshutumiwa kuwalenga waandishi wa habari na vyombo na habari, ambavyo vimeonekana kuwa wakosoaji wa mapinduzi hayo na kuweka bayana ukandamizaji unaoendelea.

Soma pia:Takriban Watu 50,000 wayakimbia makwao kufuatia mapigano kaskazini mwa Myanmar: UN

Mwaka uliopita waandishi wa habari 43 waliwekwa kizuizini, kwa mujibu wa Kamati ya Kulinda Waandishi.

Myanmar ilishika nafasi ya pili mwaka 2023 kwa kuwafunga jela waandishi wa habari, ikiwa chini ya China.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW