1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar yamkamata balozi wa zamani wa Uingereza

25 Agosti 2022

Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Myanmar Vicky Bowman na mumewe pamoja na msanii maarufu Toru Kubota wakamatwa nchini humo Alhamisi kwa madai ya kukiuka sheria za uhamiaji.

Ex-Botschafterin Uk in Myanmar Vicky Bowman
Picha: ihrb.org

Taarifa kutoka kwa utawala wa kijeshi nchini Myanmar imesema kuwa Bowman, ambaye alihudumu kama mjumbe kutoka 2002 hadi 2006, alikamatwa kwa kushindwa kutangaza kuwa anaishi katika anwani tofauti na ile iliyoorodheshwa kwenye cheti cha usajili wa wageni . Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa mumewe Htein Lin alikamatwa kwa kumsaidia mkewe kuishi katika anwani tofauti na nyumba yao iliyosajiliwa katika eneo la kibiashara la Yangon.

Msemaji wa ubalozi wa Uingereza mjini Yangon, amesema walikuwa na wasiwasi kuhusu kukamatwa kwa mwanamke Muingereza nchini Myanmar bila ya kumtaja Bowman kwa jina.

Chanzo chenye ufahamu kuhusu suala hilo kilisema Bowman na Htein Lin walipelekwa katika gereza la Insein mjini Yangon. Chanzo hicho kimeendelea kuarifu kuwa kesi ilikuwa imepangwa kusikilizwa Septemba 6, ingawa haikujulikana nini kingefanyika wakati huo.

Richard Horsey wa kundi la kimataifa la kutatua migogoro, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hiyo ilikuwa hatua ya uchokozi kutoka kwa jeshi hilo na kwamba Vicky na Htein Lin wanaheshimika sana na wamechangia mengi nchini Myanmar kwa miongo kadhaa huku akiongeza kwamba Vicky ni balozi wa zamani wa Uingereza suala linaloongeza mvuto zaidi katika kesi hiyo.

Min Aung Hlaing - Kiongozi wa jeshi la MynamarPicha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Siku ya Alhamisi, Uingereza ilitangaza vikwazo vipya kwa kampuni ambazo ilisema zimesaidia kuchangisha fedha kwa ajili ya jeshi la Myanamr wakati wa ukandamizaji wake wa mwaka 2017 dhidi ya jamii ya Warohingya walio wachache zaidi.

Idadi kubwa ya raia wa kigeni imejikuta katika msako wa utawala huo wa kijeshi kufuatia hatua yake ya kuchukua madaraka.

Mtengenezaji filamu wa Japan Toru Kubota anazuiliwa katika gereza la Insein baada ya kukamatwa mwezi uliopita karibu na mkutano wa kuipinga serikali mjini Yangon. Kubota ni mwanahabari wa tano wa kigeni kukamatwa nchini Myanmar baada ya raia wa Marekani Nathan Maung na Danny Fenster, Robert Bociaga wa Poland na Yuki Kitazumi wa Japan wote ambao baadaye waliachiwa huru na kurejeshwa nchini mwao. Kukiuka sheria ya uhamiaji nchini Myanmar kunachochea kifungo cha miaka mitano jela. Msemaji wa jeshi hilo tawala hakujibu ombi la tamko kuhusu suala hilo.

Wakati huo huo, maelefu ya waislamu wa jamii ya Warohingya leo walifanya maandamano katika kambi za wakimbizi huko Bangladesh kudai haki kutokana na msako uliofanywa dhidi yao na jeshi la Myanmar miaka mitano iliyopita .

Maandamano hayo yaliohusisha zaidi ya watu 10,000 yaliadhimisha miaka mitano ya kuhama kwa maelefu ya waislamu hao wa Rohingya kutoka Myanmar.

Viongozi wa kijamii walitoa wito wa kurejeshwa salama na kwa heshima kwa wakimbizi hao nchini mwao.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW