1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo kati ya Poland na Belarus kuendelea kwa miezi kadhaa

17 Novemba 2021

Waziri wa ulinzi wa Poland Mariusz Blaszczak amesema mzozo katika mpaka wa nchi yake na Belarus utaendelea kwa miezi kadhaa huku maelfu ya wahamiaji wakikwama katika mpaka huo wa Mashariki

Mariusz Blaszczak
Picha: imago/newspix

Katika mahojiano na redio ya taifa nchini Poland Jumatano asubuhi, Blaszczak amesema kuwa inawapasa kujiandaa na ukweli kwamba hali hiyo katika mpaka wa Belarus haitamalizika kwa utaratibu na kwamba wanapaswa kusubiri kwa miezi kadhaa wakitarajia sio miaka. Maafisa tisa wa Poland walijeruhiwa Jumanne jioni na Poland ikatumia mizinga ya maji dhidi ya makundi madogo ya wahamiaji waliokuwa wakirusha mawe kuvuka uzio wa nyaya wa mpaka.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Belarus BELTA lilisema Jumanne jioni kwamba walinzi wa mipaka walianza kuwahamisha baadhi ya wahamaiji hadi katika kituo cha mapokezi mbali na mpaka huo na hii leo, walinzi wa mpaka wa Belarus na Poland wamesema kuwa takriban wahamiaji elfu 2 walibakia katika uzio huo.

Wahamiaji katika mpaka kati ya Poland na BelarusPicha: Oksana Manchuk/BelTA/AP/picture alliance

Wakati huo huo, naibu waziri wa mambo ya ndani wa Poland Maciej Wasik amesema  kwamba wahamiaji ambao wamekuwa wakiishi katika kambi za muda katika upande wa Belarus wa mpaka huo wa Mashariki ya Poland wanasafirishwa kwa mabasi na maafisa wa Belarus na kutoa matarajio ya uwezekano wa kupungua kwa mzozo huo. Wasik amesema kuwa amepokea habari kwamba wahamiaji wamekuwa wakipanda mabasi yaliotolewa na Belarus na kuondoka katika eneo hilo

Walinzi wa mpaka wa Poland wamechapisha video katika mtandao wa twitter inayoonesha wahamiaji wakiwa na mifuko wakiongozwa na vikosi vya Belarus kutoka katika mpaka huo. Hata hivyo, msemaji wa walinzi hao wa mpakani Anna Michalska, amesema kuwa baadhi ya wahamiaji walioonekana wakibeba mbao na kuibua maswali kuhusu iwapo watahamishwa katika eneo lingine katika mpaka huo. Shirika la Belta limeripoti kuwa wahamiaji walikuwa wakipewa hifadhi ndani ya kituo kimoja katika mpaka huo na kutoa nafasi kwao kulala ndani na wala sio nje kwenye mahema baada ya siku nyingi .

Kundi kubwa la watu kutoka eneo la Mashariki ya Kati walikuwa wamekwama katika kivukio cha mpaka na Poland tangu Novemba 8 wakisubiri na kutarajia kuingia barani Ulaya. Wengi wao wanatoroka migogoro ama hali ya kukata tamaa nyumbani na kulenga kuingia Ujerumani ama mataifa mengine ya bara Ulaya. Iraq imekuwa ikitoa wito kwa raia wake kurejea nyumbani na kuwaambia kuwa njia ya kueleka Umoja wa Ulaya imefungwa. Ndege za kwanza zimepangiwa siku ya Ijumaa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW