1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo katika rasi ya Korea magazetini

15 Aprili 2013

Mzozo katika rasi ya Korea, mkutano mkuu wa chama cha upinzani cha Social Democratic-SPD, na kuibuka chama kipya cha kisiasa ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry (kushoto) na mwenzake wa China Yang JiechiPicha: Reuters

Tuanzie Mashariki ya Asia yalikokodolewa macho ya walimwengu kufuatia kitisho kinachozidi makali cha serikali ya Korea ya Kaskazini kutaka kufyatua makombora. Juhudi za kupunguza makali ya mzozo huo ndio lililokuwa lengo la ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry katika nchi tatu za Mashariki ya Asia: Korea ya kusini, China na Japan. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika:

"John Kerry alitaraji angewatanabahisha viongozi wa mjini Beijing wazidi kuwashinikiza viongozi wa Korea ya Kaskazini. Wachina lakini kwa upande wao wamewatolea wito wamarekani wazungumze ana kwa ana na Pyongyang. Pande zote mbili zimeshindwa katika juhudi zao.Wameshindwa kufikia msimamo wa pamoja kuhusu vipi wakabiliane na vitisho vinavyozidi kutolewa na Korea Kaskazini pamoja na jaribio la kombora wanalopanga kulifyetua wakati wowote kutoka sasa. Kwa namna hiyo mtu anaweza kusema katika ugomvi wa Korea, Washington na Beijing hawajafanikiwa kuijongeleza misimamo yao."

Berliner Zeitung linahisi majirani ya Korea ya Kaskazini nao pia wawajibike. Gazeti linaendelea kuandika:

"Majirani ya Korea ya Kaskazini, hata bila ya suala la kupunguza silaha,wanabidi nao pia kuchangia kurejesha uhusiano uwe wa kawaida.Kwasababu mzozo huu unawawia ghali kiuchumi na kisiasa pia. Kwa muda wote ambao mzozo huu utaendelea, Marekani na China nazo pia zitaathirika. Kwamba nchi hiyo ndogo ya Korea inayazungusha kichwa madola hayo makuu, ni ushahidi kwamba ushawishi wa Washington na Beijing una mipaka yake."

SPD wadhamiria kushinda auchaguzi mkuu

Nembo ya chama cha upinzani cha Ujerumani-Social Democratic-SPDPicha: imago stock&people

Chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani-Social Democratic-SPD kiliitisha mkutano mkuu kwa lengo la kuidhinisha mkakati wake wa uchaguzi na kwa namna hiyo kuinua hadhi yake miezi mitano kabla ya uchaguzi mkuu. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:

"Miezi mitano kabla ya uchaguzi mkuu wana SPD wanakabwa na kizungumkuti.Wanapinga muungano ule ambao wengi wa wajerumani wangeupendelea,kwasababu za kimkakati.Na hasa yeye Peer Steinbrück,mmojawapo wa mawaziri maarufu wa serikali ya muungano wa vyama vikuu,ndie anaesema yuko tayari kwa kila kitu isipokuwa kwa serikali nyengine ya muungano wa vyama vikuu.Kwa namna hiyo mgombea huyo wa kiti cha kansela kutoka SPD anawalazimisha wapiga kura wapitishe uamuzi ambao hawakupendelea kuupitisha.Wote wawili,Merkel na Steinbrück hawatoweza tena kuwa nao.Safari hii watampata mmoja tu kati yao...Huyu au yule."

Kiu cha D-Mark hakikumalizika

Konrad Adam (kushoto),Frauke Petry (kati) na Bernd Lucke wakishangiria kuundwa chama chao kipya-Chama mbadala kwa ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Na hatimae wahariri wa Ujerumani wamejishughulisha na kuchomoza chama kipya katika medani ya kisiasa humu nchini."Chama Mbadala kwa Ujerumani."Gazeti la "Donaukurier" linaandika:

Tangu jana nyota mpya imechomoza katika anga ya kisiasa humu nchini. Na kama kawaida nyota hiyo mpya inamulika muflisi wa vyama vya jadi vya kisiasa.Safari hii wanaobanwa ni wafuasi wa vyama ndugu vya CDU/CSU na kiongozi wao,kansela Angela Merkel ambae kila alichopendekeza kukabiliana na mgogoro wa fedha,kikitajwa "hakina badala".Sasa ameshampata somo: "Chama mbadala"

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW