1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa eneo la Harami Al Sharif Magazetini

Oumilkheir Hamidou
25 Julai 2017

Mzozo katika eneo tukufu kwa waislam la Haram Al Sharif , madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na matumaini ya kupungua makali mvutano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya magazetini

Israel verschärfte Sicherheitsvorkehrungen am Tempelberg in Jerusalem
Picha: Getty Images/AFP/T. Coex

 

Tunaanzia Mashariki ya kati ambako waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amebadilisha msimamo wake na kuamua ikongolewe baadhi ya mitambo ya ulinzi iliyowekwa katika milango  ya kuingia katika uwanja unakokutikana msikiti mtukufu wa Al Aqsa . Gazeti la "Rheinpfalz" linajiuliza kama waziri mkuu huyo hatobadilisha tena msimamo wake. Gazeti linaandika: "Yadhihirika kana kwamba angalao safari hii kipeo cha machafuko kinakadirika. La muhimu ni kama waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hatojiachia kwa mara nyengine tena na kuridhia shinikizo la wafuasi wa siasa kali za kizalendo. Kwa miaka sasa wanashinikiza wayahudi waruhusiwe kuingia katika eneo hilo la Harami  Al Sharif , linalotukuzwa tangu na waislam mpaka na wayahudi. Kuwaruhusu waingie katika eneo hilo lakini itakuwa sawa na kuyaendeya kinyume makubaliano ya amani ya mwaka 1994 kati ya Israel na Jordan."

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni makubwa na yanajulikana, ndio maana gazeti la "Trierische Volksfreund" linashangaa kuona kuna nchi zinazopinga kuidhinisha makubaliano yaliyofikiwa desemba mwaka 2015 mjini Paris. Gazeti hilo linaandika: "Haingiii akilini kuona kwamba katika dunia hii bado kuna watu, mfano wa rais wa Marekani Donald Trump wanaoshuku madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kuamini  eti ni kwa masilahi ya nchi zao kama hawatochukua hatua zozote kukabiliana na mabadiliko hayo. Miaka  ya 2014, 2015 na 2016 ilikuwa miaka ambayo joto lilikuwa kali kuliko wakati wowote ule mwengine ulimwenguni. Vipimo vya hali joto vilikuwa vikipindukia mwaka hadi mwaka. Na hali hiyo ina madhara yake. Na sio tu kwa madubu wa maeneo ya baridi kali ambako theluji imeshaanza kuyeyuka, kwa visiwa vidogo vidogo vilivyoko katika sehemu za mbali za dunia au kwa vijiji barani Afrika vinavyotishiwa kugeuka jangwa-madhara yake yanakutikana kote ulimwenguni, Marekani sawa na Ujerumani."

Matumaini ya kupungua mvutano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na matumaini ya kupungua mvutano kati ya Uturuki na Umoja wa ulaya. Mkutano mdogo wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Uturuki unatarajiwa kufanyika leo mjini Brussels. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika: "Malumbano makali kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yaliyoshuhudiwa mwishoni mwa wiki iliyopita, yamefuatiwa mapema wiki hii na dalili za kuibuka nia ya kutuliza hali ya mambo. Hali hiyo inatufunza kitu gani katika utaratibu wa kujiunga Uturuki na Umoja wa Ulaya? Inatufunza kwamba subira yavuta kheri na kwamba uwezekano ungalipo bado kwa Uturuki kurejea kuwa taifa linaloheshimu sheria. Mkutano mdogo wa kilele utakaofanyika leo hii mjini Brussels kati ya Uturuki na Umoja wa ulaya ni fursa nzuri."

 

Mwandishi/Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW