1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mzozo wa Gaza hauna mithili ukiangalia vifo vya wanahabari

5 Desemba 2023

Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa habari lasema vita vya Gaza vimegeuka kuwa mgogoro usiokuwa na mithili yake.

Waandishi habari wa Kipalestina wakiomboleza vifo vya wenzao Hassouna Sleem na Sary Mansour waliouawa wakati wa shambulizi Novemba 19, 2023
Waandishi habari wa Kipalestina wakiomboleza vifo vya wenzao Hassouna Sleem na Sary Mansour waliouawa wakati wa shambulizi Novemba 19, 2023Picha: REUTERS

Anthony Bellanger, ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa habari amesema kwa wastani, kila siku, mwandishi habari au mfanyakazi mmoja wa vyombo vya habari anauawa Gaza.

Takriban waandishi Habari 60 wakiwemo wafanyakazi wengine wa vyombo vya habari, wameuawa tangu vita hivyo vilipoanza Oktoba 7.

Idadi hiyo inakaribia jumla ya waandishi habari waliouawa wakati wa kipindi kizima cha vita vya Vietnam, nusu karne iliyopita.

Soma pia: UN: Mzozo wa Israel na Hamas umefikia hatua mbaya

Migogoro mingine mibaya ya Mashariki ya Kati haijakaribia kusababisha maafa mabaya kama ya sasa kwa wataalam wa tasnia ya habari.

Soma pia: Guterres: Raia wa Gaza wanakabiliwa na hali 'mbaya sana'

Akizungumza na shirika la habari la Associated press, Anthony Bellanger amesema:

"Katika vita, kama vile Syria, Iraq na iliyokuwa Yugoslavia, hatukuona aina hii ya mauaji,”

Tangu makubaliano ya kusitisha vita Gaza yaliyodumu kwa wiki moja na kumalizika Ijumaa iliyopita, maafa hayo yameendelea. Bellanger amesema kwa bahati mbaya wamepokea taarifa ya kuhuzunisha kuwa waandishi habari watatu au wanne waliuawa mwishoni mwa wiki, vita vilipoanza tena.

Kulingana na Bellanger, wanaomboleza takriban vifo vya wanahabari 60, wakiwemo 51 wa Kipalestina na wengine wa Israel na Lebanon. Wengi waliuawa wakati wa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Amesema waandishi habari wa Israel pia waliuawa wakati wa shambulizi la wanamgambo wa Hamas lililochochea vita hivyo kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7.

Amesema takwimu hizo zinatokana na vyanzo vyote ambavyo shirikisho hilo hutumia kuandaa ripoti yake ya kila mwaka.

Wanahabari wanafanya kazi katika mazingira magumu Gaza

Pamoja na idadi ya vifo, majengo mengi ya mashirika ya habari huko Gaza pia yameharibiwa.  Amekadiria kuwa kulikuwa na takriban wanahabari 1,000 na wafanyakazi wa vyombo vya habari mjini Gaza kabla ya vita, lakini sasa hakuna anayeweza kutoka.

Waandishi habari wa Kipalestina- wakiwa kazini Gaza. Oktoba 15, 2023.Picha: Momen Faiz/NurPhoto/picture alliance

Nasser Abu Baker, rais wa chama cha waandishi Habari wa Palestina, amesema licha ya waandishi habari kupoteza watu wa familia zao, majumba yao kuharibiwa, wanaendelea kufanya kazi yao hata katika mazingira magumu ya mapigano bila usalama na chakula.

Ujerumani yahimiza uwajibikaji wa kimataifa katika ukanda wa Gaza

"Mamlaka za Israel si sikivu, nimejaribu kuwasiliana na serikali ya Israel, lakini hawakuwahi kujibu. Na Nilipoenda Palestina siku chache zilizopita, nilituma pendekezo kwa ofisi ya habari kwamba tuwe na mkutano, lakini pia hakuna aliyejibu," amesema Bellanger.

Israel imesema inafanya kila juhudi kuwaepusha raia dhidi ya maafa. Nchi hiyo inalilaani kundi la Hamas kwa kuwaweka raia hatarini kutokana na kufanya shughuli zake katika maeneo ambayo raia wanaishi.

Shirika la Waandishi Habari Wasiokuwa na Mipaka IFJ limewataka waendesha mashtaka wa mahakama kuu ya jinai ICC kuchunguza vifo vya waandishi habari na wafanyakazi wa mashirika ya habari. Tayari mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Karim Khan amezuru eneo hilo.

Karim Khan ataja shambulizi la Oktoba 7, ukiukwaji wa sheria ya kimataifa

Khan ameitaka Israel na Hamas kuheshimu sheria ya kimataifa lakini alichelea kuituhumu nchi hiyo kwa uhalifu wa kivita.

Alitaja shambulizi la Oktoba 7 dhidi ya Israel lililofanywa na Hamas, kuwa ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya ubinadamu.

 

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zimeliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Katika shambulizi hilo la kusini mwa Israel, watu 1,200 waliuawa na 240 walishikwa mateka.

Baadaye Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas na kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 15,800 wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel.

Chanzo: APAE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW