Mzozo wa Gaza- Israel yatuma wanajeshi zaidi wa akiba.
12 Januari 2009Huku hayo yakijiri Juhudi za kidiplomasia bado zinaendelea ili kuutanzua mzozo huo ambao unaingia siku yake ya 16 tangu uanze Disemba 27.
Ndege 6 za kijeshi za Israel zilifanya mashambulizi dhidi ya vituo 12 vinavyodaiwa kutumiwa na wafuasi wa chama cha Hamas kufanya mashambulizi ya Maroketi dhidi ya Israel.
Mashambulizi hayo yalijibiwa vikali na Hamas katika mji Jabiliya ulioko kaskazini wa mji wa Gaza na pia katika mji wa Khan Yunis katika eneo la Kusini mwa Gaza.
Jehi la Israel lilitarajiwa kuingia katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu katika vitongoji vya mji wa Gaza vya Sheikh Anjleen.
Katika awamu hii ya tatu, Israel inasema kuwa lengo hasa ni kuharibu kabisa uwezo wa Hamas kufanya mashambulizi ya Maroketi katika ardhi yake na kwamba oparesheni hiyo huenda haitachukua muda baada ya jeshi la Israel idadi kubwa ya hifadhi na vituo vinavyotumiwa kurushia makombora hayo.
Wanawake wawili na watoto watoto wanne ni miongoni mwa raia waliouawa wakati jeshi la Israel liliposhambulia nyumba moja katika mji wa Bet Lahiya.
Mashambulizi hayo yameendelea baada ya pande hizo mbili kukataa azimio la barala la Usalama la Umoja wa mataifa, waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni akisema kuwa Israel haikushiriki katika kikao hicho kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kutambua vitendo vya kigaidi.
Rais mteule wa Marekani Barrak Obama ameitaja hali ilivyo katika eneo hilo la mashariki ya kati kuwa ya kusikitisha na inayohitaji kushughulikiwa kwa dharura na kuahidi kuwa punde tu atakapoapishwa wiki ijayo atafanya kila juhudi kukomesha vita hivyo na kuleta amani katika eneo hilo na vile vile suala la Iran.
Rais mteule Barrak Obama alisema ``Unapoona raia, wawe wa Wapalestina au Waisraeli wakiumizwa katika hali ngumu namna hii, ni jambo la kuhuzunisha sana na kuvunja moyo na bila shaka hunifanya niwe na ari zaidi ya kujaribu kuvunja mkwamo ambao umekuwa ukiendelea kwa miongo kadhaa´´
Hatua hiyo imepongezwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ambayo akekuwa katika eneo hilo tangu wiki iliyopita kusaidia juhudi za kutafuta amani baina ya pande hizo mbili.
Steinmeier alisema kuwa anamatumaini makubwa kuwa viongozi wa kiarabu wataafikiana na Israel, akiongeza kuwa ipo haja ya kufungwa kwa njia zinazotumiwa kupitisha silaha kimagendo katika maeneo ya mpakani.
Baada ya mashauriano na rais Hosni Mubaraka anayeongoza mashauri ya amani katika eneo hilo, Steinmeier alisema kuwa serikali ya Ujerumani iko tayari kutoa msaada katika juhudi za kusimiwa kwa eneo la mpakani la Misri.
Zaidi ya Wapalestina 900 wauawa tangu vita hivyo vianze disemba 27 huku Israel ikiwapoteza wanajeshi wake 13 na raia 3. Vita hivyo vimesababisha maandamano makubwa katika miji mbali mbali ya Ulimwengu.
Pande hizo mbili zinazozonaza zilikatalia mbali azimio la Umoja wa mataifa wiki iliyopita uliozitaka kukomesha mara moja mapigano, na kuondoka kwa jeshi la Israel katika ardhi ya Gaza.
Matumaini ya kuutanzua mzozo huo sasa yamesalia kwa mpango wa amani unaoongozwa na misri ambapo wajumbe wa pande hizo mbili wanatarajiwa mjini Cairo kuendeleza mashauriano hayo.
Israel ilisema kuwa haijali itakavyochukuliwa na jamii ya kimataifa, na itaendelea na mashambulizi hayo hadi pale itakapohakikisha kuwa hakuna maroketi yanayorushwa kutoka upande wa Gaza.
Kwa upande wake Hamas ilisema kuwa azimio hilo haliwezi kutekelezwa kwasababu haikuwakilishwa katika kikao hicho. Hata hivyo kunahabari kuwa huenda mashauriano yanayoongozwa na Misri yakafanikiwa.