1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa gesi kati ya Russia na Ukraine ni somo kwa umoja wa Ulaya

Josephat Charo5 Januari 2006

Mzozo wa gesi kati ya Russia na Ukraine katika siku chache zilizopita haukuzishughulisha tu nchi hizo mbili, lakini pia bara la Ulaya. Kampuni la Gazprom linalodhibitiwa na ikulu ya Kremlin liliposhindwa kukubaliana juu ya bei ya gesi na serikali ya Kiev, liliamua kukatiza kupeleka gesi nchini Ukraine. Hatua hiyo iliyaathiri mataifa kadhaa barani Ulaya.

Kwamba mzozo huo wa gesi ungeweza kutokea tena, sio jambo linaloweza kuwa kama onyo kwa Ulaya. Usalama wa kuendelea kuwepo nishati ya pamoja kwa mda mrefu ni jambo linalotakiwa kupewa kipaombele.

Je umoja wa Ulaya imeamshwa kutoka usingizini? Je mzozo wa gesi kati ya Russia na Ukraine utasababisha athari kwa kiwango gani? Hatimaye vuta ni kuvute hii imesababisha wasiwasi mkubwa katika mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya na kiwango cha gesi katika mifereji kimepungua kwa karibu aslimia hamsini.

Mzozo huu wa gesi uliodumu kwa siku chache umefanyika kwa wakati unaofaa. Umoja wa Ulaya unatakiwa ufahamu kwamba ni lazima ujiandee kukabiliana na upungufu wa nishati wakati wa mizozo ya aina hiyo. Muongozo wa umoja wa Ulaya kuhusu swala hilo ulitupiliwa mbali mwaka wa 2004. Ni kweli kwamba muongozo huo ulipendekeza kila taifa lichukue hatua zake binafsi, lakini matokeo yaliyojitokeza kufikia sasa yanadhihirisha kwamba ufanisi uliopatikana katika taifa moja haukupatikana katika mataifa mengine.

Kwa sababu umoja wa Ulaya unategemea sana ununuzi wa nishati kutoka nje, mashindano katika masoko ya nishati yataendelea kuongezeka. Hatimaye mataifa yanaoyoinukia kiuchumi yaliyo na mafuta na gesi kama vile China na India yatakabiliwa na wasiwasi. Athari zinazoweza kusababishwa na hali hii zilidhihirika mwishoni mwa mwaka jana. Iwe ni katika vituo vya kuuzuia mafuta au mahala pa kuchemshia maji, bei za mafuta ya petroli, mafuta yaliyosafishwa, na spiriti ziliongezeka sana.

Kwa hiyo huu ni wakati mwafaka wa kulitilia maanani jambo hili na kuangalia vipi umoja wa Ulaya utakavyojiandaa kukabiliana na mizozo juu ya nishati haba kama vile gesi. La muhimu lakini ni kwamba mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya sharti yakubali kwamba yanakabiliwa yote kwa pamoja na tatizo hili, yawe hivi sasa yana mafuta au gesi kutoka pwani au nchi kavu au yawe hayana kitu.

Lakini kufikia sasa swala hili haswa halipo. Kwa mfano Uingereza haitaki kushinikizwa na Brussels ieleze vipi inavyotumia nishati yake. Hilo sio jambo la muhimu sana. Ukweli ni kwamba umoja wa Ulaya ni lazima utafute njia vipi mataifa wanachama yataweza kusaidiana wakati taifa moja litakapokatiza kwa mda mfupi usafirishaji wa nishati kwa taifa moja katika umoja huo.

Kitu cha muhimu zaidi ambacho lazima kifanywe kwa haraka ni kuunda mkakati utakaofaa kwa kipindi kirefu. Je itawezekana vipi kupunguza hali ya kuyategemea mataifa yanayomiliki mafuta mengi kama vile Russia, Saudi Arabia na Iran? Haya ni mataifa ambayo yote kwa pamoja hayaungi mkono mawazo ya mataifa ya magharibi ya ustawi na demokrasia na ambayo mara kwa mara yanaweza kushindwa kusafrisha mafuta.

Ndio maana kamishna wa kawi wa halmashauri ya umoja wa Ulaya, Andris Piebalgs hafanyi makosa anapopendekeza swala la nishati lipewa uzito mkubwa katika ajenda ya umoja wa Ulaya. Kwa njia hii umoja huo unaweza kujikokota na kujikakamua kuyafikia malengo yake. Jambo hili linataka kuwepo na umoja katika muelekeo wa siku za usoni katika siasa ya nishati, na kwa sasa mambo hayaonekani kuwa mazuri hivyo.

Ijapo Ufaransa imeamua kubakia na vinu vyake vya nyuklia, na Uingereza kwa upande wake ikiwa na nishati yake ya gesi na mafuta, lazima ifahamike kwamba nishati ya upepo, maji na jua zitatoa mchango mkubwa. Ndio maana swala la kuchanganya aina mbalimbali za nishati ni lazima lijadiliwe kwa haraka.

Austria ambayo inashikilia uraisi wa umoja wa Ulaya tayari imeanza kuliangalia swala hili. Yenyewe ikiwa ni nchi yenye uhaba wa nishati ingependelea kuendeleza siasa ya nishati katika kiwango cha umoja wa Ulaya.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW