Mzozo wa gesi kati ya Urusi na Belarus
23 Juni 2010Kiasi hicho ni sawa na punguzo la asilimia 60 ya matumizi yote ya siku. Hali hiyo imesababishwa na deni la kiasi cha dola milioni 192 la malipo ya mafuta ya Belarus.Kwa upande wake Belarus inashikilia kuwa inaidai kampuni ya nishati ya Urusi ,Gazprom kiasi cha dola milioni 200 kama malipo ya kusafirishia gesi hadi mataifa mengine ya Ulaya. Katika mkutano na maafisa wa ngazi za juu, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya nishati ya Urusi ya Gazprom,Alexei Miller aliitangaza hatua hiyo ya kuipunguzia kiasi cha gesi kinachoifikia Belarus.Hata hivyo bado kiasi cha gesi inayosafirishwa kupitia Belarus bado hakijabadilika wakati yote hayo yakiendelea.
Punguzo maradufu
Hapo jana,Urusi iliamua kuipunguzia Belarus maradufu kiasi cha gesi inayoihitaji kwa siku.Mwanzoni mwa wiki hii punguzo hilo lilikuwa asilimia 15.Mkurugenzi wa kampuni ya nishati ya Urusi,Gazprom Alexei Miller anasisitiza kuwa Belarus kamwe haijachukua hatua zozote za kulilipa deni inalodaiwa.
Urusi imeonya kuwa punguzo hilo litaendelea sanjari na deni hilo ambalo kwa sasa linaripotiwa kuwa kiasi cha dola milioni 192.Deni hilo limelimbika tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi mwezi wa Aprili.Endapo Urusi italiongeza deni la mwezi wa Mei kiasi hicho huenda kikafikia dola milioni 250.
Wakati huohuo kulingana na maafisa wa serikali ya Belarus,mataifa ya eneo la Ulaya ya Magharibi bado yanaendelea kupata gesi inayotokea Urusi bila ya matatizo yoyote hata baada ya Rais Alexander Lukashenko kutishia hapo jana kuisimamisha shughuli hiyo.Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Belarus,kampuni yake ya kusafirishia gesi ya Beltransgaz , imeamriwa kuhakikisha kuwa mfumo wake mzima unafanya kazi bila ya vikwazo vyovyote kwa minajili ya kuyakimu mahitaji ya wateja wake.Mkurugenzi wa Shirika la Gazprom Alexei Miller alisema kuwa'',Tunajitahidi kufanya kila tuwezalo ilikuhakikisha kuwa wateja wetu wa bara la Ulaya hawaathiriki kwa njia yoyote ile.''alieleza.
Wanadaiana?
Hapo jana Jumanne,maafisa wa serikali za Belarus na Urusi walilijadili suala la madeni wanayodaiana.Rais Lukashenko alilirejelea tena ombi lake la kuongezewa muda wa kuzitafuta dola milioni 192 inazodaiwa na Urusi.Belarus inadai kuwa tayari imeshailipa Urusi kiasi kisichojulikana cha matumizi ya mwezi wa Mei.Wakati huohuo Belarus inadai kwamba Urusi haijailipa kiasi cha dola milioni 260 kama malipo ya kusafirishia gesi kwa kipindi cha miezi mitano ya mwanzo wa mwaka huu.
Huku mzozo huo ukiendelea,mataifa hayo mawili yametangaza kuwa ushirikiano kati yao katika suala la nishati umeimarika.Kwa mujibu wa Waziri wa nishati wa Urusi Sergei Shmatko aliyezungumza na shirika la habari la ITAR-Tass,nchi yake inajiandaa kuzuwia matatizo yoyote kuwafikia wateja wake wa mataifa ya Ulaya magharibi.Hatua hizo zinajumuisha kuwa na waangalizi wasioegemea upande wowote wakati wa usafirishaji pamoja na mauzo ya gesi.
Awali mivutano ya gesi kati ya Urusi na Ukraine iliyasababisha mataifa ya Ulaya kutokuwa na bidhaa hiyo muhimu hususan katika msimu wa baridi.Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umeuondoa wasiwasi huo kwa kiasi cha asilimia 6.25 ya gesi yote inayohitajika barani Ulaya inatokea Belarus.Msemaji wa Idara ya mambo ya nje katika Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Marlene Holzner ,''Hatuna taarifa zozote zinazoeleza kuwa huduma za gesi zimesitishwa katika taifa la Lithuania.Endapo hilo limetokea basi basi kama tulivyosema Latvia itaisafirishia gesi hiyo kwakiopindi cha wiki moja.Kwa sasa,hatuwezi kujua kitakachotokea baada ya wiki hii ,''amelieleza hilo.
Chachu ya mvutano
Ifahamike kuwa mataifa ya Lithuania,Poland na Ujerumani yanaitegemea gesi ya Urusi inayosafirishwa kupitia Belarus.
Kulingana na vyombo vya habari vya Urusi,mvutano huo umesababishwa na Belarus inayoipinga hatua yake ya kuanzisha ushurikiano wa forodha itakayoijumuisha pia Kazakhstan.Waziri wa mambo ya nje wa Belarus,Sergei Martynov,anaripotiwa kueleza kuwa nchi yake inataka halmashauri hiyo kuwapa washirika wote haki sawa.Kiongozi huyo aliyasema hayo hapo jana Jumanne alipokutana mjini Minsk na mwenzake wa Urusi.Wachambuzi nao wanaeleza kuwa mzozo huo unachagizwa na hali kwamba Belarus inajisogeza karibu zaidi na Umoja wa Ulaya kinyume na ilivyokuwa awali ikishirikiana kwa karibu zaidi na Urusi.
Huku yote hayo yakiendelea,mazungumzo ya suluhu kati ya pande mbili husika yanatarajiwa kuendelea hii leo.
Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE
Mhariri:Josephat Charo