1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Iran bado waendelea

Saumu Mwasimba6 Agosti 2008

Nchi za Magharibi zaikataa barua ya Iran na sasa watafuta vikwazo zaidi dhidi ya nchi hiyo

Iran yasema urutubishaji wa madini ya Uranium hausitishwiPicha: AP

Marekani na washirika wake wa Ulaya wameikataa barua ya hivi karibuni ya Iran kuhusiana na mpango wake wa nuklea na sasa wanapigania vikwazo vipya vya kiuchumi vya baraza la usalama la umoja wa mataiafa dhidi ya Iran.

Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani , China na Urusi zitakua na mazungumzo leo juu ya hatua itakayofuata baada ya kupokaea barua ya Iran, iliokua na jibu la pendekezo lao la kuipa msaada wa kiuchumi na kiufundi, ikiwa kwa upande wake itasitisha mpango wake wa nuklea.

Lakini kwa mujibu wa magazeti ya Washington Post na New York Times, msemaji wa Marekani katika ubalozi wake kwenye Umoja wa mataifa Ric Grenell ni kwamba barua hiyo imeshakataliwa, akitamka" pendekezo letu liko wazi lakini lakini jibu lao si wazi."

Akaongeza kwamba Iran inapaswa kutoa jibu lililowazi kabisa kuhusiana na ridhaa hiyo ambayo alisema ni ya jumuiya ya kimataifa.

Ripoti ya magazeti hayo imesema Marekani na washirika wake wa Ulaya sasa watarudi kwenye baraza la usalama kutaka vikwazo zaidi dhidi ya Iran ambayo inakataa kusitisha urutubishaji wa madini ya uranium, hatua moja muhimu katika utengenezaji wa bomu la nuklea.

Iran bado inasema iko tayari kuendelea na mazungumzo ya kusaka suluhisho.

Katika barua yake kwa mataifa 6 yenye nguvu yaani matano yalio wanachama wa kudumu wa baraza la usalama na Ujerumani, Iran imesema" kwa nia njema, muelekeo wa maana na mkakati imara na kujitolea kuendelea na mazungumzo, tumezingatia vizuri kwa mara nyengine maoni yaliyoelezwa katika mazungumzo ya Geneva ili kuleta makubaliano madhubuti ya ushirikiano, ambayo yataweza kusawazisha wasi wasi wetu wa pamoja na kuwa msingi wa haja yetu ya kushirikiana pamoja na kuweka ajenda ya mashauriano ili kufikia makubaliano yatakayokubaliwa na wote.

Barua hiyo pamoja na mengine ikasisitiza kwamba duru ya pili ya mashauriano inaweza kuanza tena ikiwa kuna nia kama hiyo kutoka upande wa pili.

Hata hivyo kutokana na kukataaliwa kwa barua hiyo na Marekani na washirika wake wa Ulaya, kuanza kwa duru ya pili ni kugumu katika wakati ambao Marekani na washirika wake hao wanawania kulitaka baraza la usalama kuiwekea Iran vikwazo zaidi.

Marekani na washirika wake wa ulaya watajiunga na China na Urusi kwa njia ya simu katika mazungumzo hayo kuamua hatua itakayofuata.

Wakati huo huo naibu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Atomiki la umoja wa mataifa Olli Heinonen ataelekea Iran kesho kwa mazungumzo zaidi kuhusu mpango wake wa Nuklea.

Lakini afisa mmoja wa kibalozi katika makao makuu ya Shirika hilo mjini Vienna ambaye hakutaka kutajwa jina alisema ziara hiyo ya Bw Heinonen haihusiani moja kwa moja na matukio hayo ya karibuni kuhusu jibu la Iran, bali ina lengo la kutaka kupata ufafanuzi juu ya masuali yaliobakia juu ya malengo hasa ya Iran.

Iran inashikilia kwamba mpango wake wa nuklea ni kwa ajili ya nishati tu na sio jengine.