1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Iran na Marekani wahamia nchini Iraq

Sekione Kitojo
30 Desemba 2019

Wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran wamesema idadi ya watu waliofariki kutokana na shambulio la jeshi la Marekani nchini Iraq na  Syria dhidi ya wapiganaji wao imepanda na kufikia watu 25, na kuapa kulipiza.

Irakische Sicherheitskräfte während Militäreinsatz n auf der Suche in der Provinz Anbar
Picha: Reuters/T. Al-Sudani

Wanamgambo  hao  wamesema  watalipiza kisasi  kutokana na  mashambulio hayo  ya  uovu yaliyofanywa  na  kile  walichosema ni Wamarekani wasiojitambua.

Kikosi cha wanamgambo wa Hezbollah nchini Iraq kikijitayarisha kwa mapambanoPicha: picture-alliance/AP Photo

Shambulio  la  Marekani , likiwa  ni shambulio  kubwa  kabisa  hadi hivi  sasa  lililolenga  wanamgambo  wanaoungwa  mkono  na serikali  nchini  Iraq , na  miito  ya  kulipiza  kisasi, inawakilisha ongezeko  jipya  la  vita vya  mataifa  mengine  vinavvyopiganwa nchini  humo kati ya  Marekani, na Iran zinazofanya mapambano  yao katika  mashariki  ya  kati  ambayo yanaweza  kutishia  maslahi  ya Marekani  katika  eneo  hilo.

Miito  ya  kutaka  kulipiza  kisasi  mjini  Baghdad  imekuja  siku  moja baada  ya  waziri  wa  ulinzi  wa  Marekani  Mark Esper  kusema Marekani  imefanya  mashambulio  hayo ya  kijeshi  na  kulenga wanamgambo  wa  Iraq  wanaoungwa  mkono  na  Iran, ambao inawalaumu  kwa  shambulio  la  roketi  ambalo  lilisababisha  kifo cha  mkandarasi  Mmarekani  nchini  Iraq wiki  iliyopita.

Waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Marekani  Mike Pompeo amesema  mashambulizi hayo  yanatuma  ujumbe  kuwa  Marekani haitavumilia  hatua  zinazofanywa  na  Iran  kuhatarisha  maisha  ya Wamarekani.

Kikosi cha jeshi nchini Iraq kinachofahamika kama "vikosi vya umma vya mapambano" vyenye wapiganaji kutoka kwa jamii ya WashiaPicha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Mashambulizi yaliyopangwa

Jeshi  la  Marekani  lilisema "Mashambulizi yaliyopangwa na  kulenga kwa  usahihi" yalifanywa  dhidi  ya  maeneo  matano ya  Kataeb Hezuboullah, ama  vikosi  vya  Hezbollar nchini  Iraq  na  Syria. Kundi hilo, ambalo  ni  jeshi tofauti kutoka  kundi  la  kijeshi  la  Hezbollah nchini Lebanon, linafanya  shughuli  zake  chini  ya  mwamvuli  wa wanamgambo  wanaoungwa  mkono  na  serikali  wanaofahamika kwa  jumla  kama  majeshi  ya  umma  ya  kuhamasisha. Wengi  wao wanaungwa  mkono  na  Iran.

"Vita  vyetu na  Wamarekani  na  mamluki wao  sasa  vimefunguliwa kwa uwezekano  wote," Kataeb Hezbollah  limesema  katika taarifa usiku  wa  Jumapili.

"Hatuna  chaguo  leo  mbali  ya  kupambana na  hakuna  ambacho kinaweza  kutuzuwia  kutolipiza  kisasi kwa  uhalifu  huu."

Marekani  inawalaumu  wanamgambo hao  kwa  mashambulizi  ya maroketi  siku  ya  Ijumaa  ambayo  yalisababisha  mkandarasi  wa wizara  ya  ulinzi  ya  Marekani  katika  eneo  la  kijeshi  karibu  na Kirkuk, kaskazini  mwa  Iraq, pamoja  na  mashambulizi  mengine kadhaa  katika  vituo vya  vikosi  vya  Marekani  nchini  Iraq ambavyo  hakuna  kundi  lililodai  kuhusika  nayo.Maafisa wanasema  zaidi ya  maroketi 30 yalifyatuliwa  katika  shambulio  la Kirkuk.

Mpiganaji wa kikosi cha wanamgambo nchini Iraq akijaribu chombo cha kufyatulia magurunetiPicha: picture-alliance/AP Photo/M.Brabu

Msemaji wa  kataeb Hezbollah  alikana  kuwa  kundi  hilo linahusika na  mashambulizi  hayo  ya  maroketi dhidi  ya  vituo  vya  Marekani, ikiwa  ni  pamoja  na  moja  ambalo  lilisababisha  kifo  cha mkandarasi  wa  Marekani, wakisema  Marekani  inatumia mashambulizi  hayo  kama njia  ya  kulishambulia  kundi  hilo.