1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Iran na Marekani wajadiliwa na Umoja wa Ulaya

Oumilkheir Hamidou
13 Mei 2019

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo amewasili Brussels kuzungumzia makubaliano kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran wakati Uingereza inatoa onyo kali dhidi ya kuripuka mzozo" bila ya kutaka" katika Ghuba."

EU-Iran Handel | Federica Mogherini und Javad Zarif
Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/Li Muzi

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo amepangiwa kukutana , pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, na mawaziri wenzake wa  Uingereza, Ufaransa na Ujerumani-madola matatu yaliyotia saini makubaliano ya mwaka 2015 yaliyoikatisha Iran matumaini ya kutengeneza silaha za nuklea ili badala yake iondolewe vikwazo.

Iran ilitangaza wiki iliyopita inasitisha utekelezaji wa baadhi ya vifungu vya makubaliano hayo, mwaka mmoja baada ya uamuzi wa rais Donald Trump wa kujitoa pamoja na kutangaza vikwazo vikali zaidi dhidi ya jamhuri hiyo ya kiislam.

Mbali na mvutano wa kidiplomasia rais Trump ameamua pia kutuma manuari ziada za kivita katika ghuba. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza Jeremy Hunt ametoa wito wa "kuwepo kipindi cha utulivu na kuonya dhidi ya hatari ya kuiona Iran ikirejea upya katika enzi za kutengeneza silaha za nuklea.

Mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya bibi Federica Mogherini amesisitiza umuhimu wa kuendelezwa mazungumzo kama njia pekee bora ya kumaliza mivutano na kuepusha hali kuzidi kuwa mbaya katika eneo la Ghuba.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema hatua ya Marekani ya kupitisha vikwazo dhidi ya Iran "si za manaufaa kwao".

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: DW/M. Luy

Makubaliano ya mradi wa nuklea wa Iran ni muhimu kwa usalama barani Ulaya

Pembezoni mwa mazungumzo ya mawaziri 28 wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani watakutana na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kuzungumzia jinsi ya kuendeleza makubaliano ya mradi wa nuklea wa Iran.

"Sisi barani Ulaya tunakubaliana makubaliano haya ni muhimu kwa usalama wetu. Hakuna anaetaka kuiona Iran ikimiliki bomu la nuklea. Na hilo ndilo lengo la makubaliano hayo na hilo limeweza kufikiwa hadi sasa. Ndio maana tutaendeleza kila juhudi kuhakikisha makubaliano yanatekelezwa."Amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko Maas.

Mbali na Iran , mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya watajadili pia hali namna ilivyo nchini Libya, na kubadilishana maoni kuhusu kikao kitakachoitishwa hivi karibuni kati yao na mawaziri wa mambo ya nchi za nje na wale wa ulinzi kutoka mataifa matano ya kanda ya Sahel, ambayo ni pamoja na Burkina faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa/

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW