Qatar yasema mateka zaidi kuachiwa
28 Novemba 2023Pande hizo mbili zilikubaliana kurefusha muda wa kusitisha vita hadi kesho Jumatano huku kukiwa na mipango miwili ya kuwaachia mateka wanaoshikiliwa na Hamas na kwa upande wa Israel kuwaachia wafungwa wa Kipalestina walioko katika magereza ya Israel.
Hali hiyo inatizamwa kuwa mbinu ya Hamas kuchelewesha kurejea kwa vita vya Israel. Wakati huo huo shinikizo linaongezeka kwa Israel kuwaepusha raia wa Palestina dhidi ya mashambulizi wakati itakapoanza upya mashambulizi yake huko Gaza.
Qatar ambayo inahusika pakubwa na juhudi za upatanishi imesema lengo na matumaini ya wajumbe kwenye makubaliano kati ya Israel na Hamas kwa sasa ni kuendeleza kusimamishwa mapigano ili kuyapa nafasi mazungumzo zaidi.
Fahamu zaidi kuhusu mateka wa Israel chini ya Hamas
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed al-Ansari amesema kulingana na makubaliano inategemewa Hamas kuwaachilia mateka 10 kwa kila siku ya ziada ya usitishaji vita.
Qatar: Usitishaji zaidi wa vita unategemea Hamas kuachia mateka
"Hadi sasa tuna uhakika kuwa mateka 20 wataachiliwa kati ya Jumanne na Jumatano. Bila shaka ndani ya saa 48, kutakuwa na juhudi za kurefusha muda zaidi wa usitishaji mapigano. Lakini hilo pia itategemea ikiwa Hamas wataachilia mateka zaidi," amesema al-Ansari.
Je Mzozo wa Israel na Hamas utaathiri vipi mkutano wa COP28?
Israel imeahidi mara kwa mara kuwa punde itakapokuwa dhahiri kuwa hakuna mateka zaidi watakaoachiliwa huru chini ya makubaliano ya sasa, itarejea vitani ili kuangamiza Hamas, kundi ambalo pamoja na nchi nyingine ikiwemo Marekani hulitaja kuwa la kigaidi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekariri wito wake wa kusimamishwa vita kwa muda mrefu na kuachiliwa huru kwa mateka wote.
Olaf Scholz aahidi serikali yake yashinikiza kuachiwa kwa mateka wote
Naye kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameahidi kuwa serikali yake imejitolea kikamilifu kuhakikisha mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas huko Ukanda wa Gaza wanaachiwa huru.
Kupitia taarifa ya serikali kwa bunge la Ujerumani siku ya Jumanne, Scholz ameelezea kuwa amefarijika juu ya kuachiwa baadhi ya mateka katika siku za hivi karibuni.
Kutokana na kwamba Wajerumani ni miongoni mwa mateka walioachiliwa, Scholz amesema hiyo ni sababu nyingine ya kufurahia.
Usitishaji vita waibua matumaini ya mateka zaidi kuachiwa
Hamas pamoja na wanamgambo wengine wanawashikilia takriban mateka 160 kati ya 240 waliowakamata walipofanya shambulizi la kigaidi mnamo Oktoba 7 kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200.
Antony Blinken kurudi Mashariki ya Kati
Katika tukio jingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, anatarajiwa kurudi tena Mashariki ya Kati mwishoni wiki hii kutafutia mzozo huo ufumbuzi zaidi.
Hiyo itakuwa mara ya tatu Blinken anafanya ziara hiyo tangu vita hivyo vilipoanza, na anatarajiwa kushinikiza kuendelezwa kwa usitishaji vita na kuachiwa huru kwa mateka zaidi.
Kulingana na takwimu za wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya Wapalestina ambao wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel tangu vita vianze imefikia 13, 300.
Utawala wa rais wa Marekani Joe Biden umeiambia Israel kwamba ni sharti iepushe uhamishaji mkubwa wa watu na maangamizi ya watu wengi miongoni mwao raia wa Palestina ikiwa itarudi vitani.
Mnamo Jumatatu, mateka 11 waliachiliwa huru na kufanya jumla ya mateka ambao wameachiliwa huru kufikia sasa kufika 51. Israel vilevile imewaachilia wafungwa 150 wa Palestina.
Bonyeza hapa upate makala zaidi kuhusu mzozo wa muda mrefu wa Mashariki ya Kati
Vyanzo: APAE, DPAE