Mzozo wa Katalonia na wimbi la mrengo wa kulia Magazetini
23 Oktoba 2017Tunaanzia Uhispania na mvutano unaozidi makali kati ya serikali kuu mjini Madrid na wanaopigania kujitenga jimbo tajiri la Katalonia. Mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" anahisi waziri mkuu Mariano Rajoy hakuwajibika ipasavyo.Gazeti linaendelea kuandika: "Mariano Rajoy hakuutumia muongozo wa sheria kwa tahadhari na wala si kwa busara. Angebidi kwanza awawekee mawaziri wa jimbo hilo, wasimamizi ili kuzuwia hatua zozote nyengine kuelekea uhuru. Angepigania kuwapokonya nyadhifa zao tu pindi wangebisha. Anaetaka kuuhami mfumo wa taifa linaloheshimu sheria, anabidi binafsi aheshimu ipasavyo mfumo huo. Jibu la Rajoy kwa waasi wa Katalonia ni mchanganyiko wa kusikitisha wa hali ya kusita sita na pupa."
Rajoy ndie wakulaumiwa
Maoni sawa na hayo yametolewa na mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anaeandika: "Rajoy hajatathmini kwa makini na tahadhari mwongozo wa sheria. Kuanzia November mwaka 2015 alikuwa akijua kwamba wanaopigania kujitenga jimbo la Katalonia, hawafanyi maskhara. Siku hiyo ndipo bunge la jimbo hilo lilipotangaza azma ya kuendelea na utaratibu wa kujitenga na Uhispania. Rajoy hakufanya chochote kaachia mambo yaendelee. Na tangu wakati huo amebakia kujibu tu na nadra kwa kutumia hikma."
Mrengo wa kulia waenea Ulaya
Mada yetu ya pili magazetini inamulika wimbi la siasa kali za mrengo wa kulia linalopiga barani Ulaya. Baada ya Austria, na nchi jirani ya Cheki pia imemchagua mfuasi wa siasa kali za mrego wa kulia ashike hatamu za uongozi. Hata hivyo gazeti la "Allgemeine Zeitung"lina maoni tofauti na linaandika: "Kijuu juu tu ndipo mtu anapoweza kusema kwamba kundi jipya limeibuka katika sehemu ya mashariki mwa ulaya. Kundi la wahafidhina wanaofuata siasa kali za kizalendo wanaotawala kuanzia Poland hadi kufikia Hungary na hivi karibuni pengine nchini Austria. Hata hivyo mshindi wa uchaguzi katika jamhuri ya Cheki Andrej Babis si mfuasi wa siasa kali za kizalendo mfano wa Kaczynski wa Poland au Orban wa Hungary. Na wala hana fasaha kama Kurz wa Austria. Ni tajiri tu anaepigania masilahi yake."
Kilio cha wakinamama
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na kashfa ya kudhalilishwa wanawake wanapokuwa wanatafuta kazi au wanataka kupanda cheo. Gazeti la "Rhein-Nevker-Zeitung" linaandika: "Ni viziri kuona kwamba baadhi ya warembo mashuhuri wa Hollywood wamepiga moyo konde na kufichua hadharani yaliyowafika. Hayo yanawapa moyo wanawake wengine pia ambao si mashuhuri kama wao, wazungumzie na wao pia yaliyowasibu. Hatua nyengine lakini itabidi iwe kutosubiri miaka kadhaa ipite, hadi unapohakikisha kazi yako haiko tena hatarini, kwasababu hilo linawapa nguvu wanaofanya madhila hayo.
Mwamdishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri