1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Kisiasa huko Schleswig- Holstein, jimbo la Ujerumani.

Halima Nyanza17 Julai 2009

Chama cha Kansela wa Ujerumani, cha Christian Democrats, CD, katika jimbo la Schleswig-Holstein, kimepiga kura kusitisha ushirikiano wake na chama cha Social Democrats -SPD-, baada ya kutoelewana kati ya viongozi wake.

Viongozi wa vyama SPD na CDU, vilivyo katika serikali ya shirikisho la Ujerumani katika jimbp la Schleswig-Holstein, Ralf Stegner wa SPD (kushoto) na Peter Harry Carstensen wa CDU, ambao wapo katika malumbano.Picha: AP


Miezi miwili kabla ya kufanyika uchaguzi wa Shirikisho la Ujerumani, Waziri Mkuu wa jimbo la Schleswig-Holstein, Peter Harry Carstensen, ambaye anatokea chama cha -CDU, amesema wabunge 30 kutoka chama hicho cha CDU wamepiga kura kwa kauli moja kuimaliza miaka minne ya serikali ya shirikisho kabla ya uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika Mei mwakani.


Ameengezea kwa kusema kuwa jimbo hilo linahitaji serikali imara.


Lakini, hata hivyo, chama cha SPD ambacho kina viti 29 bungeni, kinapinga hatua hiyo, na kwamba kitahakikisha kuwa chama cha CDU hakifikii theluthi mbili ya kura itakayowezesha kuvunjwa bunge, katika zoezi la kupiga kura linalotarajiwa kufanyika Jumatatu. Ni hapo kutaamuliwa kuuvunja ushirikiano huo ama la.


Naye kiongozi wa wabunge wa CDU katika bunge hilo la jimbo la Schleswig-Holstein, Johann Wadephul, amepinga kulazimisha kuwepo serikali hiyo ya mseto.

Kwa upande wake, kiongozi wa wabunge wa Chama cha SPD katika jimbo hilo, Ralf Stegner, amesema hakuna sababu ya kulivunja bunge la jimbo.

Amesema iwapo waziri mkuu anaweza kujiuzulu.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema mabishano katika jimbo hilo la kaskazini kabisa mwa Ujerumani hayaelekei kuleta madhara kwa uchaguzi wa nchi nzima ya Ujerumani hapo Septemba 27, ambapo Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, anawania nafasi ya kuiongoza nchi hii kwa awamu ya pili.


Mtaalamu wa siasa katika Chuo Kikuu cha Bonn, Gerd Langguth, anasema suala hilo la kisiasa katika jimbo la Schleswig-Holstein halitaathiri serikali ya Shirikisho la Ujerumani, zaidi ya kuwakumbusha watu kwamba ushirikiano ni mgumu.


Vyama hivyo viwili vya CDU na SPD vinatawala kwa pamoja katika serikali ya mkoa wa Schleswig-Holstein iliyokuwa katika hali ngumu tangu mwaka 1995.



Mwandishi: Halima Nyanza(ARD/Reuters)

Mhariri: Othman, Miraji