Mzozo wa Madagascar
13 Machi 2009Hatma ya Rais Marc Ravalomanana iko mashakani hasa baada ya kuonekana akiomba ulinzi kutoka kwa wafuasi wake, baada ya kuibuka taarifa kuwa wanajeshi waasi wanajitayarisha kuingia mji mkuu wa Antananarivo. Mgogoro wa uongozi kati ya Ravalomanana na mpinzani wake wa kisiasa, Andry Rajoelina, umesababisha vifo vya zaid ya watu 100 tangu mwezi Januari.
Rais Ravalomanana amefikia kiwango cha kuomba usaidizi wa wafuasi wake, kufuatia mgogoro huo wa uongozi nchini Madagascar. Kulingana na duru kutoka baadhi ya wanadiplomasia, vifaru va kijeshi vimeingizwa katika kambi ya kijeshi ya Capsat katika mji mkuu wa Antananarivo, tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza. Kambi ya kijeshi ya uasi dhidi ya rais Ravalomanana ilianza kujikusanya mwishoni mwa wiki.
Hatua hiyo ya wapinzani ilimfanya rais Ravalomanana kukosa uamuzi ila kuwaita wafuasi wake akiwaambia waje katika ikulu yake wamlinde hii ni baada ya walinzi wake wa awali kutoroka ikulu.
Madagascar imezama kwenye mgogoro wa kisiasa tangu Januari baada ya meya wa zamani wa Antananarivo, Andry Rajoelina, kuanzisha upinzani dhidi ya utawala wa Ravolamanana unaoshtumiwa kuitawala nchi hiyo kwa mabavu. Tangu wakati huo Rajoelina amefanikisha maandamano kote Madagascar kutaka Ravalomanana ajiuzulu madarakani.
Jumapili, jeshi la Madagascar lilizidisha unga katika maji pale walipoasi, na kuanza kukataa kutii amri za rais wakimshtumu kwa jinsi anavyotumia nguvu kupita kiasi kuzima machafuko na maandamano ya raia nchini humo. Uasi huo umesambaa katika kambi nyingi za kijeshi, na ingawa mkuu wa majeshi alitishia kuwa huenda jeshi likatwaa uongozi wa nchi hiyo iwapo Ravalomanana na mpinzani wake Rajoelina hawataafikiana kuzima mzozo huu wa kisiasa wadadisi wa mambo wanasema hii haimanishi jeshi linamuunga mkono Rajoelina wa upinzani.
Balozi wa Marekani kisiwani Madagascar Niels Marquardt alinukuliwa kusema kwamba anahofu ya kuzuka vita kutokana na hali ilipofikia lakini amewashauri raia wa Marekani nchini humo kuondoka.
Jamii ya kimataifa imekuwa ikitaka paweko mazungumzo ya upatanishi kati ya pande zinazozozana nchini Madagascar, lakini juhudi hadi sasa zimeambulia patupu. Upinzani umekuwa ukilalamika kwamba Ravalomanana aliye uongozini kwa miaka saba sasa, ametawala kimabavu, ameuangusha uchumi wa Madagascar na sasa hawana imani naye, hivyo ang'atuke mamlakani, ili kuundwe serikali ya mpito itakayoongozwa na Rajoelina.
Ravalomanana mapema wiki hii alikubali hadharani kuwa kweli amefanya makosa kadhaa katika utawala wake, lakini amekataa kata kata kuondoka madarakani, akisisitiza alipewa madaraka alipoteuliwa kwa muhula wa pili mwaka wa 2006 kuwa rais wa Madagascar.
Mwandishi: Munira Mohammaed/AFP
Mhariri: Miraji Othman