1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa madeni upatiwe ufumbuzi haraka

29 Novemba 2011

Rais wa Marekani Barack Obama ametoa mwito kwa viongozi wa Ulaya kuchukua hatua za dhati kuumaliza upesi, mzozo wa madeni unaohatarisha kanda nzima ya sarafu ya euro na hata ukuaji wa kiuchumi nchini Marekani.

Rais Barack Obama wa Marekani ahimiza hatua za dhati kumaliza mzozo wa madeni barani UlayaPicha: dapd

Rais Obama jana alisisitiza umuhimu wa kuharakisha kupata suluhisho litakaloumaliza mzozo huo wa madeni barani Ulaya. Alipozungumza mjini Washington baada ya kukutana na Rais wa Baraza la Ulaya Herman Van Rompuy, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, na mkuu wa sera za nje za umoja huo, Bibi Catherine Ashton, alisema Marekani ipo tayari kujitolea ili kusaidia kuumaliza mzozo huo. Akaongezea kuwa masoko dhaifu barani Ulaya yataathiri nafasi za ajira nchini Marekani. Licha ya kutumia diplomasia hadharani, kuna ishara kuwa Obama wakati wa mazungumzo yake na viongozi hao wa Umoja wa Ulaya, alikuwa na msimamo mkali. Kwani kuna hofu kuwa mzozo wa kanda ya euro unaweza kuongeza matatizo ya kiuchumi nchini Marekani, ambayo tayari yanazusha wasiwasi juu ya uwezekano wa Obama kuchaguliwa tena mwaka 2012.

Wakati huo huo, msemaji wa Ikulu ya Marekani mjini Washington, Jay Carney alieleza hivi:

" Huu ni mzozo wa Ulaya - na Ulaya ina uwezo wa kuushughulikia mzozo huo. Hatuamini kuwa msaada zaidi unahitajiwa kutoka Marekani, yaani kutoka walipa kodi wa Marekani."

Njia moja ya kusaidia kuleta utulivu barani Ulaya ni kwa Marekani, kuongeza mchango wake katika shirika la fedha la kimataifa IMF ambako tayari ni mfadhili mkubwa kabisa. Lakini Balaozi wa Marekani katika Umoja wa Ulaya, William Kennnard ameipinga kabisa fikra hiyo. Amesema na ninanukuu: "Nataka kueleza waziwazi. Hakujafanywa majadiliano yoyote kuhusu suala la Marekani kuongeza mchango wake katika IMF au ahadi zo zote zile za kutoa msaada wa fedha kwa Umoja wa Ulaya katika ufumbuzi wa mzozo huo" mwisho wa kunukuu.

Rais Barack Obama (kati) pamoja na Rais wa Baraza la Ulaya Herman Van Rompuy(shoto) na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel BarrosoPicha: dapd

Baada ya kuwa na mkutano huo na Rais Obama, Van Rompuy alieleza kuwa Umoja wa Ulaya hivi sasa unapitia kipindi kigumu, lakini akazitetea hatua zinazochukuliwa kurejesha ukuaji wa kiuchumi ambazo hapo awali wala zisingezingatiwa. Hata hivyo, amesema bado wanahitaji kuchukua hatua zaidi.

Wakati huo huo, mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya euro leo wanakutana mjini Brussels kukubaliana njia ya kuuimarisha mfuko wa kuzisaidia nchi zenye madeni katika kanda ya euro ulio maarufu kama EFSF.

Mwandishi: Martin,Prema

Mhariri:Miraji Othman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW