Mzozo wa uhamiaji waitikisa serikali ya Merkel
19 Juni 2018Hali hiyo inatishia kuiporomosha serikali ya muungano inayoongozwa na kansela Merkel ambayo imedumu kwa muda wa miezi mitatu hadi sasa.
Wakati huo huo Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanapambana kuweza kupata msimamo wa pamoja katika mageuzi ya Umoja huo kabla ya mkutano muhimu mwishoni mwa mwezi huu ambao unaweza kuelekeza hatima ya kundi hilo mla mataifa.
Chama cha jimbo la Bavaria cha Christian Social Union , CSU, kina wasiwasi wa kupoteza wapiga kura kwa chama kipya cha siasa kali za mrengo wa kulia katika uchaguzi wa jimbo mwezi Oktoba, na kinataka pachukuliwe hatua ya kupiga marufuku wahamiaji kuingia nchini Ujerumani kwa wale waliokwisha andikishwa katika nchi nyingine ya Umoja wa Ulaya.
Rais wa Marekani Donald Trump, akitetea sera zake kali dhidi ya wahamiaji, aliingilia katika mjadala wa Ujerumani jana kwa kuandika katika ukurasa wa Twitter akikosoa sera za Merkel za kufungua mipango kwa wahamiaji, kwamba ni makosa makubwa, kwamba sera hizo zimechochea uhalifu barani Ulaya. Kiongozi wa chama cha CSU, Horst Seehofer, alikubali mjini Munich kuchelewesha kuweka marufuku ya kuingia katika jimbo hilo hadi baada ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya tarehe 28 hadi 29 Juni, kumpa muda zaidi Merkel kutafuta suluhisho la jumla kwa mataifa ya Umoja huo.
Merkel anapinga hatua yoyote ya peke yake inayoweza kuchukuliwa na waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha CSU, ambayo itabadilisha sera yake ya kufungua milango kwa wahamiaji ya mwaka 2015 na kudhoofisha mamlaka yake.
Maadili ya pamoja Ulaya na Marekani
Ulaya na Marekani hazina maadili ya pamoja, msemaji wa serikali ya Ufaransa amesema leo wakati hasira ikiongezeka kuhusiana na sera ya utawal wa rais Trump ya kuwatenga wazazi wahamiaji na watoto wao wanaowasili kutoka katika mpaka na Mexico.
Mtafaruku kuhusiana na watoto waliowekwa kizuwizini unatokana na sera za rais Donald Trump za kutovumilia kabisa wahamiaji, ambamo wahamiaji wanakamatwa wanapoingia Marekani kinyume na sheria na wanashitakiwa kwa uhalifu.
Seneta wa Marekani Ted Cruz kutoka jimbo la Texas amezungumzia kuhusu sakata hilo nchini Marekani, hali ambayo inaleta mtafaruku duniani.
"Sisi wote ambao tumeona picha za watoto wakiondolewa kwa mama na baba zao wakilia, tunajisikia vibaya sana. Hali hii ni lazima isitishwe. Wiki hii nitawasilisha mswada wa sheria ambao unawalinda watoto na wazazi wao ambao utawala ammlaka watoto kuishi na wazazi wao. Na pia utaondoa mashitaka. Sababu ya haya kutokea ni kwamba kuna kesi nyingi za uhamiaji."
Kansela Angela Merkel atakuwa na mkutano leo na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa mazungumzo ya pamoja kuhusiana na mageuzi ya Umoja wa Ulaya, hususan masuala muhimu ya uhamiaji ambayo yanaligawa kundi hilo la mataifa na kuweka mbinyo katika siasa za ndani ya Ujerumani kwa Markel.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Josephat Charo