1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaushambulia mji wa Ukraine wa Vinnytsia.

15 Julai 2022

Siku moja baada ya shambulio la kombora la Urusi lililosababisha vifo vya watu 23 katika mji wa Ukraine wa Vinnytsia, mzozo huo kati ya mataifa hayo mawili unaendelea kusababisha uhaba wa chakula na nishati duniani kote.

Ukraine Krieg Angriff auf Winnyzja
Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Ukraine imesema shambulio hilo la makombora katika mji wake wa Vinnytsia liliendeshwa kutoka kwa manowari ya Urusi iliyopo katika Bahari Nyeusi. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliitaja Urusi kuwa ni taifa la kigaidi na kuhimiza vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Kremlin na kusema idadi ya vifo huko Vinnytsia inaweza kuongezeka.

Nayo Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema jengo lililoshambuliwa lilikuwa linatumiwa kwa mkutano kati ya maafisa wa kijeshi na wasambazaji wa silaha za kigeni na kuwa shambulio hilo lilipelekea kuwatokomeza washiriki wa mkutano huo.

Mzozo huo wajadiliwa katika mkutano wa G20

Vita vya Urusi nchini Ukraine vilitawala pia ajenda katika mkutano wa leo wa mawaziri wa fedha wa G20 nchini Indonesia. Fuko la fedha la kimataifa IMF linataka kuwepo mipango ya kuwasaidia 'walio hatarini zaidi'. Mkurugenzi mkuu wa fuko hilo Kristalina Georgieva anasema kuwa ulimwengu unakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.

"Tunakabiliwa na mkusanyiko wa matatizo ambayo sidhani kuwa tumewahi kukutana nayo. Tulikuwa na janga la kwanza (la COVID 19), ambalo lilisisitisha uchumi wa dunia na kutusukuma kwenye mdororo wa kiuchumi. Vita vya Ukraine, vimezua mshtuko mwengine wa kiuchumi kabla hata ya ule wa kwanza kumalizika, na hivyo kuongeza kasi ya mfumuko wa bei uliokuwa umeanza hapo awali."

Mzozo huu unahusisha mataifa mawili ambayo ni wauzaji wakuu duniani wa nafaka, mafuta na gesi na umesababisha uhaba wa chakula na nishati, mfumuko wa bei, mgogoro wa kifedha na huenda ukasababisha pia baa la njaa.

Makubaliano kuhusu usafirishaji wa nafaka

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya ulinzi ya Urusi amesema leo kuwa "hati ya mwisho" iliyoundwa ili kuruhusu tena usafirishaji wa nafaka kutoka bandari ya Ukraine katika Bahari Nyeusi itakuwa tayari "hivi karibuni", kufuatia mazungumzo na Ukraine wiki hii mjini Istanbul nchini Uturuki.

Mazungumzo ya Istanbul ambayo yaliandaliwa ili kupunguza mzozo wa chakula duniani, yalifanyika siku ya Jumatano na yalihusisha maafisa wa Umoja wa Mataifa na Uturuki na yalikuwa mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine tangu mwezi Machi.   Soma zaidi:  UN: Tunatarajia bidhaa zitaanza kupita Bahari Nyeusi

Umoja wa Ulaya umesema utapiga marufuku uagizaji wa dhahabu ya Urusi katika awamu ya saba ya vikwazo dhidi ya utawala wa Kremlin iliyopendekezwa leo Ijumaa mjini Brussels nchini Ubelgiji.

Uamuzi wa Rais wa Urusi Vladmir Putin wa kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine mwezi Februari umetatiza usafirishaji wa nafaka katika bandari za Ukraine na hivyo kuzidisha mzozo wa chakula duniani kote hasa ikizingatiwa kuwa Ukraine ni mojawapo ya wauzaji wakubwa wa ngano duniani.

(AFP,RTRE, DPAE)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW