1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Venezuela na Marekani wazidi kufukuta

12 Desemba 2025

Hatua ya hivi karibuni ya Marekani kuikamata kwa meli kubwa ya mafuta karibu na pwani ya Venezuela kwa madai ya usafirishaji wa dawa za kulevya inaashiria kuwa suluhisho baina ya mataifa hayo halipo karibu kupatikana.

Marekani St. Petersburg 2025 | Maandamano dhidi ya operesheni ya kijeshi ya Marekani katika Karibiani
Rais wa Marekani Donald Trump na Nicolás Maduro wa Venezuela wanahusika katika mzozo unaokua kwa kasi.Picha: Dave Decker/ZUMAPRESS/picture alliance

Katika miezi ya karibuni, Rais Donald Trump ametuma maafisa wa ujasusi kwa siri ndani ya Venezuela, wanajeshi na ndege za kivita, na kuamuru kuzamishwa meli zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya, hujuma ambayo imesababisha vifo kadhaa.

Uhusiano kati ya Marekani na Venezuela uliharibika tangu Hugo Chávez, shujaa wa rais wa sasa Nicolas Maduro, alipochaguliwa mwaka 1999.

Baada ya jaribio la mapinduzi la 2002, Venezuela ilimfukuza balozi wa Marekani. Baada ya kifo cha Chávez mwaka 2013, Maduro alichukua madaraka.

Machado alipokea Tuzo ya Amani ya Nobel 2025.Picha: Stian Lysberg Solum/AP Photo/picture alliance

Mwaka 2019, Marekani ilimuunga mkono mpinzani mkubwa wa Maduro, Juan Guaidó, na kusababisha mgawanyiko wa kimataifa. Maduro alichaguliwa tena 2024, huku María Corina Machado akizuiwa kugombea kwa tuhuma za ufisadi ambazo waangalizi wengi waliziona ni za kubuni.

Machado alipokea Tuzo ya Amani ya Nobel 2025 na anaonekana kuwa chaguo linalotarajiwa iwapo Maduro ataondolewa madarakani.

Msimamo wa Marekani

Lakini Maduro anasema Marekani inataka mabadiliko nchini mwake kwa kutumia vitisho vya kijeshi. Trump kwa upande wake amesema "siku za Maduro zinahesabika” lakini hakukanusha uwezekano wa uvamizi wa jeshi la ardhini dhidi ya Caracas.

 

Nicolás Maduro amekuwa rais wa Venezuela tangu mwaka 2013.Picha: Pedro Mattey/Anadolu/picture alliance

Katika biashara, tangu 2019, mali za serikali ya Venezuela nchini Marekani zimezuiwa. Venezuela ina akiba kubwa ya mafuta ghafi , lakini vikwazo vya Marekani vimeizuia kuuza rasilimali yake hiyo katika masoko makubwa ya kimataifa, na kuilazimisha kuuza kwa bei ya chini kwa China.

Badala yake Marekani inayodai kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini Venezuela, inaonekana sasa kutumia nguvu za kijeshi kama njia moja ya kupambana dhidi ya wale inaowaita "magaidi wa dawa za kulevya,” ingawa uhalali wake umetiliwa mashaka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW