1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano ndani ya chama CDU

26 Oktoba 2015

Mzozo wa wakimbizi barani Ulaya, Maandamano kupinga chuki dhidi ya wageni Cologne, na kasheshe ya maandalizi ya kombe la dunia la kabumbu nchini Ujerumani mwaka 2006 ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi magazetini

Wakimbizi katika mpaka wa Austria na SloveniaPicha: Reuters/L. Foeger

Tuanzie lakini na mzozo wa wakimbizi na hasa na matokeo ya mkutano wa dharura wa kilele wa viongozi wa Umoja wa ulaya mjini Brussels:Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:"Viongozi wa serikali na taifa hawakufanya chochote chengine isipokuwa kujaribu kurekebisha hali ya mambo inayodhihirika kuvurugika:Sio kwanza waachiwe kuingia,ili baadae watenguliwe na halafu warejeshwe walikotokea.Lakini kwanza wachunguzwe,baadae waruhusiwe kuingia wale wenye haki ya kupatiwa kinga ya ukimbizi.Hilo ndilo jambo ambalo Ulaya inabidi ilifanye.Na fikra hiyo ingekuwa ya maana bila ya haka kama ingefikiriwa mapema.

Mzozo wa wakimbizi unaleta mfarakano hata miongoni mwa wanachama wa chama cha kansela Merkel ,Christian Democratic Union.Gazeti la "Münchner Merkur linaandika:"Vigogo wa chama wananguruma,lakini hawaandai mapinduzi dhidi ya kiongozi wao .Kwa sasa hakuna anaeweza kukamata nafasi ya mshika bendera wa chama hicho.Zaidi ya hayo Angela Merkel si mtu mwenye kukubali kushindwa na mnamo siku za nyuma ametoa dalili muhimu za kisiasa-kuundwa maeneo ya mpito karibu na mpakani au kuzidishwa makali sheria za kuwarejesha walikotokea-ikilazimika hata kwa msaada wa jeshi la shirikisho-Bundeswehr,wale ambao maombi yao ya kinga ya ukimbizi yatakataliwa.Marekebisho yanayotajwa chamani yameanza kutekelezwa na kansela hatua baada ya hatua.Na zaidi ya hayo,wanaonung'unika chamani wanatambua fika,makelele yao yanakidhoofisha pia chama chao kama ilivyodhihirika katika utafiti wa maoni ya wanchi hivi karibuni. Asilimia 36 tu wanasema kwa sasa wangekipigia kura chama cha CDU-idadi ndogo kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu miaka mitatu iliyopita.Kila wakimbizi wanapoingia kwa wingi ndipo nao wapiga kura walio wengi wanapoendelea kuvipa kisogo vyama ndugu vya CDU/CSU.

Maandamano ya amani dhidi ya chuki Cologne

Mada nyengine iliyochambuliwa magazetini ni maandamano makubwa yaliyoitishwa jana katika jiji la Cologne kupinga yale yaliyoitishwa na makundi ya siasa kali wanaopinga wageni na dini ya kiislam -Hogesa. Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger linaandika:Cologne inaonyesha upepo unavuma wapi.Wakaazi wa jiji la Cologne wana kila sababu ya kuwa na fahari na mji wao.Maelfu wameandamana kwa amani dhidi ya wafuasi wa siasa kali 1000 na matumizi yao ya nguvu.Hatuwaachii hata upenu mdogo wafuasi wa siasa kali-ndio kauli mbiu ya maandamano hayo yaliyochanganyika na burudani.Hata polisi wameridhika,wameidhibiti vyema hali katika maandamano ya pande zote mbili.

Kasheshe ya dimba la dunia 2006 lawazungusha vichwa mashabiki

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na suala eti kweli uamuzi uliopelekea Ujerumani kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2006 ulikuwa wa hadaa? Gazeti la "Emder Zeitung" linaandika:"Ni ujinga kuamini kwamba michuano ya fainali ya kombe la dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani haikununuliwa. Lakini hadi wakati huu unakosekana ushahidi wa dhana za hongo. Kuna tuhuma nzito nzito tu na kuna matamshi ya mwenyekiti wa shirikisho la dimba la Ujerumani DFB-Wolfgang Niersbach.Matamshi hayo yanaabishana na yale ya amtangulizi wake Theo Zwanziger.Jambo pekee thabiti linalojulikana hadi wakati huu ni kitita cha Euro milioni 6.7 zilizomiminwa katika kasha ambalo mpaka sasa bado halijabainika.

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW