Mzozo wa wakimbizi wawasumbuwa viongozi wa Italia
8 Agosti 2017Tunaanzia Italia ambako viongozi wanalalamika, Umoja wa Ulaya hawawasaidii kulipatia ufumbuzi tatizo la wakimbizi. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika:"Serikali ya Italia inawashinikiza walio nyuma yao katika orodha ya waliozidiwa katika mzozo huu wa wakimbizi.....Mashirika ya misaada ya kiutu. Umoja wa Ulaya umekaa kimya wala haujitahidi kusaka ufumbuzi wa kuaminika. Ufumbuzi huo unajulikana ingawa hauungwi mkono kisiasa na pia ni shida kuutekeleza. Badala ya kuwatenga moja kwa moja, unahitajika utaratibu halali wa kuwasajili, maombi ya ukimbizi yadurusiwe haraka iwezekanavyo na watakaokataliwa warejeshwe nyumbani bila ya kupoteza wakati. Kwa wakati wote ambao utaratibu huo hautatekelezwa, Italia itaendelea kukabwa na mzozo wa wakimbizi na Umoja wa Ulaya utakuwa ukikodowa macho tu bila ya kujua la kufanya."
Kizungumkuti cha mvutano pamoja na Uturuki
Vipi kuushughulikia mvutano pamoja na Uturuki ni mada nyengine iliyochambuliwa na wahariri wamagazeti ya ujerumani.Gazeti la "Südwest Presse" linaandika: "Erdogan hataki kusikia lawama. Pengine anafuata mkakati wake ule ule wa kiburi na dharau: raia wa Ujerumani wasiokuwa na hatia wanashikiliwa kama rehani ili kulazimisha maafisa wa kijeshi wa Uturuki walioomba kinga ya ukimbizi nchini Ujerumani warejeshwe nyumbani. Mwenye kufuata sera kama hizo zisizothamini utu, hoja hazimshituwi. Sasa mtu kama huyo watu wakae naye vipi? Kumtenga moja kwa moja haitosaidia kitu.
Kwa sababu wanaoshikiliwa nchini Uturuki hawatoweza kusaidiwa ikiwa njia zote za mazungumzo zitafungwa. Na pia kwa wajerumani wenye asili ya Uturuki wanaoishi humu nchini, malumbano ya moja kwa moja hayatosaidia kitu isipokuwa kuzidisha makali ya misimamo yao. Muhimu ni shinikizo la kiuchumi na maazungumzo. Angalao pamoja na wale Waturuki wanaopendelea kuwa na Uturuki ya aina nyengine na sio ile ya rais Erdogan."
Hatima ya Nicolas Maduro na Venezuela
Mzozo wa Venezuela unazidi makali. Nini au nani anaweza kumzuwia rais Nicolas Maduro, linajiuliza gazeti la "Volksstimme" linaloendelea kuandika: "Mambo matatu yanaweza kumwangusha Rais Nicolas Maduro: Mapinduzi ya kijeshi, ghadhabu za wananchi au kupoteza uungaji mkono wa washirika wake. Kimsingi Maduro alikuwa tayari awe ameshang'olewa madarakani - watu wakitilia maanani hali ya maisha namna ilivyo: ughali wa maisha umefikia asili mia 1000 na ufukara unazidi kuenea.
Kwamba ghadhabu za wananchi si kubwa hivyo, hilo linasababishwa na mchanganyiko wa nguvu za kisiasa na kijeshi. Yeyote yule ambae ni afisa wa ngazi ya juu wa kijeshi na anajitajirisha kupitia mashirika ya umma, hatoipindua serikali. Uasi wa kijeshi wa jumapili iliyopita ni tukio la kipekee. Imesalia njia ya tatu: Marekani na mataifa jirani yamevunja Ushirikiano pamoja na Venezuela.
Lakini bima ya maisha kwa Maduro ni uhusiano wake pamoja na washirika wake wakubwa, Urusi na China. Kama ilivyo katika kadhia ya Korea ya kaskazini wanamuunga mkono kwasababu anaiangalia Marekani kuwa ni "adui mkubwa."
Kwa namna hiyo mtu anaweza kusema Maduro hatikisiki madarakani, angalao kwa sasa."
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef