Mzozo wazuka upya kati ya AFC/M23
17 Novemba 2025
Wakati Kinshasa inasisitiza kuwa inataka kurejesha shughuli za uwanja wa ndege kabla ya mwisho wa mwaka, AFC/M23 wanasema uamuzi huo ni wa upande mmoja na hauheshimu makubaliano ya usimamizi wa pamoja yaliyotiwa saini katika mchakato wa DohaKati ya mvutano huu wa kisiasa, mamia ya watu waliokuwa wakitegemea shughuli zao karibu na uwanja wa ndege wanasema wako katika hali ngumu na wanahofia mustakabali wao.
Huko Goma, uwanja wa ndege wa kimataifa haukusimamisha tu shughuli za safari za ndege. Umesimamisha pia maisha ya mamia ya watu. Tangu kufungwa kwake, wafanyabiashara wadogo, wabeba mizigo na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi waliokuwa wakiishi kutokana na shughuli za uwanja wa ndege wanaendelea kujikongoja kwa shida. Na makubaliano ya Doha ambayo yalionekana kuleta matumaini, sasa yanaonekana kufufua tena mvutano.
Jumamosi iliyopita, Kinshasa na AFC/M23 walitia saini itifaki nane, zikiwemo zile za usimamizi wa pamoja wa maeneo bado yaliyoko chini ya udhibiti wa waasi. Miongoni mwa matangazo makuu ya serikali : kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Goma kabla ya mwisho wa mwaka. Lakini uamuzi huo haukubaliki upande wa M23.
Kati ya tafsiri hizi mbili zinazokinzana, mchambuzi mmoja ,ambaye alitaka kubaki bila kutajwa jina, anajaribu kufafanua hali hii ya mkwamo. Kwa mujibu wake, kutokubaliana huku kuhusu kufunguliwa kwa uwanja wa ndege kunaonyesha mvutano wa nguvu unaoendelea kati ya serikali ya Kongo na AFC/M23 licha ya makubaliano ya Doha.
"Kwa M23, jambo hili halikubaliki. Kwao wao, kufungua benki kungekuwa na kipaumbele zaidi kuliko kufungua uwanja wa ndege. Hatujui ni nani yuko sahihi, lakini ni wananchi wanaopoteza katika hali hii. Serikali, kwa upande wake, inasisitiza kuwa uwanja wa ndege ndio unapaswa kufunguliwa kwanza. Kila upande unavuta upande wake. Tunaomba pande zote mbili wakae pamoja na kuleta hatimaye amani ya kudumu ambayo tumekuwa tukiiingojea.”
Raia wanahisi kutelekezwa
Na katika uhalisia wa maisha, wananchi wanahisi kutelekezwa. Familia nyingi ziliishi kwa kutegemea shughuli zinazohusiana na uwanja wa ndege, kama ilivyo kwa Albertine Ciruza. Mjane na sasa bila ajira, anaona matumaini yake ya kurejea kazini yakitoweka.
"Kwangu mimi, haya makubaliano ni mizaha tu. Wananchi hawajawahi kuwa kiini cha maamuzi. Nilipoteza kazi yangu uwanja wa ndege ulipofungwa. Nilikuwa naitunza familia yangu. Leo tunakula kwa shida. Tulikuwa na matumaini kutokana na makubaliano haya… lakini inaonekana kila kitu kimepangwa ama kwa faida ya M23 au ya serikali ya Kinshasa.”
Katika kipindi hiki cha mvutano kati ya Kinshasa na AFC M23 kufunguliwa kwa uwanja wa ndege, badala ya kuwa ishara ya kuanza kwa uwezeshaji wa uchumi, kumekuwa uwanja mpya wa mvutano wa kisiasa.
Mazungumzo yajayo yanapaswa kubainisha hatua, kalenda na mifumo ya utekelezaji wake kwa kushirikisha mamlaka za eneo, jadi na taasisi halali za serikali.