1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nüremberg yaongoza Bundesliga

Ramadhan Ali21 Agosti 2006

Mabingwa Bayern munich na makamo-bingwa Werder Bremen walitamba mwishoni mwa wiki.usukani wa Lihi lakini umo mikononi mwa Nüremberg.Wanariadha wa afrika watamba katika Grand Prix huko Monaco na Angola ni timue pekee ya Agfrika kuwika katika ubingwa wa dunia wa basketball hujko Japan.

Bayern Munich yaizaba Bochum 2:1
Bayern Munich yaizaba Bochum 2:1Picha: AP

Mabingwa watetezi wa Ujerumani Bayern Munich waliikomea jana Bochum mabao 2:1 wakati makamo bingwa Werder Bremen, walitoka nyuma na kuitoa Bayer Leverkusen kwa mabao 2:1.Nuremberg, inayoongoza orodha ya Ligi iliikomea Borussia Mönchengladbach bao 1:0 na kuparamia kileleni mwa Bundesliga.

Roy Makay ndie aliewafungulia mlango mabingwa Bayern Munich kabla beki mshahara Philipp Lahm, kutia bao la ushindi dhidi ya Bochum,timu iliopanda daraja ya kwanza msimu huu.Katika changamoto ya pili jana, Stuttgart iliizaba Armenia Bielefeld mabao 3-2.

Huko Spain, mabingwa wa ulaya FC Barcelona walitoroka na kombe lao la kwanza msimu huu baada ya kuirarua Espanyol kwa mabao 3:0 katika duru ya pili ya finali ya Super cup nchini Spian.Barcelona inayocheza na Ronaldinho wa Brazil na Samuel Eto’o wa Kamerun, ina miadi na Sevilla katika finali ya Kombe la Ulaya la Super Cup ijumaa hii.

Katika premier League-kombe la Ligi la Uingereza, Wayne Rooney,alipiga hodi mara 2 na kuitiwa karibu katika lango la Fulham na mwishoe Manchester ilianza msimu mpya kwa mshindo wa mabao 5-1.

Mabingwa Chelsea, pia walianza kwa mshindo mkubwa walipoikandika Manchester City mabao 3:0.

Kocha wa Chelsea,Jose Mourinho,ametoa changamoto kwa timu yake ioneshe kwamba yaweza kuvumilia vishindo vya kutetea ubingwa wao tena msimu huu.

Mchezaji wa timu ya taifa ya Mali,Mahamadou Diarra, atajiunga na Real Madrid ya spian kwa mkataba wa miaka 5 kutoka klabu bingwa ya Ufaransa Olympique Lyon.

Mjumbe wa Afrika katika Halmashauri kuu-tendaji ya FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni,Ismail Bhamjee kutoka Botswana, alijiuzulu jana kutoka wadhifa wake huo .Bhamjee, aligunduliwa akiuza tiketi 12 kwa bei ya juu mara tatu kwa mashabiki wa Uingereza kabla ya changamoto kati ya Uingereza na Trinidad na Tibago, wakati wa kombe la dunia hapa Ujerumani mwezi Juni.

Bhamjee ambae kitendo chake hicho kilisababisha kufukuzwa kwake katika Kombe la dunia na rais wa FIFA Sepp Blatter, alikuwa amalize wadhifa wake katika halmashauri kuu-tendaji ya FIFA mwishoni mwa mwaka huu,kufuatia kushindwa kuchaguliwa upya.

Bhamjee amejiuzulu pia wadhifa wake mwengine kama mjumbe wa heshima wa CAF-shirikisho la kabumbu la Afrika na ataacha pia madaraka ya mwenyekiti wa COSAFA-shirikisho la dimba la kusini mwa Afrika hapo Oktoba.

Ismail Bhamjee,alitimuliwa nje ya chama cha mpira cha Botswana mwishoni mwa wiki iliopita kufuatia mjadala motomoto.

Akijieleza ilikuaje akauza tiketi za kombe la dunia kwa mashabiki wa Uingereza, Bhamjee, alisema tu azma yake ilikuwa kuwasaidia mashabiki waliokuwa na kiu kikubwa cha tiketi aliokutana nao hotelini.

Wengi wangejiuliza-mbona alipandisha bei ya tiketi mara tatu katika kusaidia huko au Bhamjee alijisaidia mwenyewe ?

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la Afrika la vijana duru ya kwanza, Malawi iliilaza Lesotho 2:0 na inasonga mbele kwa ushindi wa mabao 3:2 kufuatia duru zote mbili.Kenya ilikumtwa bao 1:0 na Rwanda na Rwanda yaiacha Kenya nyuma kwa mabao 2:0.Gabon yaitandika Nigeria 2:0,lakini ni chipukizi wa Nigeria, wanaocheza duru ijayo kwa ushindi jumla wa mabao 3:2.

Gambia iliitoa Morocco kwa 2:0 na inasonga mbele kwa ushindi jumla wa mabao 4:2.

Kombe la Tusker kwa mara ya kwanza limekwenda upande usiotazamiwa:Kagera.Kwani Kagera sugar, walitoroka jana na kombe hilo katika finali ya kusisimua ajabu walipoivua taji mabingwa Simba ya Tanzania.Kagera walinguruma kwa mabao 2:1.Dakika 1 ikisalia,Simba ikiongoza kwa bao 1:0:Kagera ikasema, „kutangulia,si kufika.“ Walisawazisha na kurefusha mchezo.Mwishoe waliipiga kumbo Simba na kuondoka kombe.

Katika medani ya riadha,majogoo wa Afrika mashariki waliwika katika mashindano ya Grand prix huko Monaco: Muafrika kusini, Mbulaeni Mulaudzi, alitamba katika mbio za mita 800 wanaume kwa muda wake wa 1:44.14 akifuatwa nafasi ya pili na mkenya William Yiampoy.

Katika changamoto ya mita 1.500 Alex Kipchirchir pia wa Kenya alinyakua ushindi akifautwa na mmorocco Mohammed Moustaoui.

Abraham Chebii aliipatia Kenya ushindi mwengine katika mita 3000 huku Hicham Bellani wa Morocco akibidi kuridhika na nafasi ya pili.Yusuf Biwott wa kenya alimaliza watatu.

Mkenya Jeruto kiptum alimaliza wa 3 katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi –ushindi ukienda kwa mbelurusia Alesya Turova.

Tumalizie mashindano ya ubingwa wa dunia wa „basketball“- mpira wa kikapu huko Hiroshima,Japan:

Mabingwa wa Afrika Angola, walitiimua nje New Zeland kwa mabao 95-73 hii leo na hivyo, wameingia hatua ya kupigana kumbo-knock-out.Timu nyengine za Afrika hazikufua dafu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW