Na Charles Hilary Mpango mpya wa Geneva ambao unatazamiwa kuzinduliwa jumatatu ijayo kwa ajili ya Mashariki ya Kati ...
27 Novemba 2003Matangazo
una makusudi ya kukomesha machafuko na ghasia katika eneo hilo,ambapo Wapalestina watakuwa na kuwa na haki ya wakimbizi wao milioni 3.8 kusamehewa na kurejea katika maeneo yao ya zamani na pia watarejeshewa maeneo yao yote ya Ukingo wa Magharibi,huku umiliki wa mji wa Jerusalem utakuwa wa mgawano baina ya Israel na Palestina. Mataifa ya kiarabu kwa ujumla yameupokea kwa mikono miwili mpango huo wa Geneva kama ni suluhisho jipya la amani kwa eneo la Mashariki ya Kati,lakini hapo hapo zinahofia kwamba kutakuwa na mabadiliko madogo kwa upande wa Palestina kwa vile tu Waziri Mkuu wa Israel Ariel Sharon ataendelea kubakia madarakani. Misri na Jordan nchi pekee za Kiarabu zilizoweza kufikia muafaka wa amani na Israel,zimeunga mkono mpango huo huku Waziri Mkuu wa Israel Ariel Sharon akiukataa.Mpango huo ulitangazwa katikati ya mwezi uliopita mjini Jordan,ambapo aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria wa Israel Yossi Beilin na Waziri wa Zamani wa Habari wa Palestina,Yasser Abed Rabbo waliongoza mazungumzo hayo ya kutayarisha yatakayoafikiwa na pande zote mbili. Rais wa Palestina Yaseer Arafat ameuunga mkono mpango huo wa Geneva,lakini akasita kuuidhinisha kwa vile Israel inazidi kuuwekea vizingiti.Bwana Arafat alisikika akisema Oktoba 4 katika kauli yake ya kwanza tangu mpango huo upitishwe,kwamba sio makubaliano rasmi.Alisema pia sio sera za Palestina kuzuia jaribio lolote la kufikia makubaliano ya amani,kama alivyofanya na bwana Rabin,akiwa na maana aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel marehemu Yitzak Rabin,ambao wote kwa pamoja walipewa nishani ya amani ya Nobel mwaka 1993 mjini Oslo. Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina Ahmed Qure8i naye amesema anasubiri kuona Israel itakuwa na jibu gani kuhusiana na mpango huo kabla ya kueleza msimamo wake bayana,ingawa mwenzake wa Israel bwana Sharon tayari anaupinga mpango huo. Hata hivyo mbunge mmoja katika bunge la Palestina Hassan Kreisheh amesema ni dhahiri Rais wao Bwana Arafat alikuwa nyumba ya maandalizi ya mpango huo wa Geneva na viongozi wengine wa Palestina,ingawa kuna hoja kwamba Mawaziri wa Palestina hawakuwa wameshirikishwa katika mazungumzo ya kuandaa mpango huo. Nae Waziri Mkuu wa Israel,Ariel Sharon amebainisha leo kwamba ni dhahiri Israel itatakiwa kuachia baadhi ya maeneo ya ardhi wanayoyakalia,lakini ameapa kuendeleza,tena kwa kasi ujenzi wa ukuta ambao umekuwa ukipigiwa kelele na Jumuia ya Kimataifa,kwa sababu Sharon amesema ukuta huo ndio utakuwa kikwazo kwa Wapalestina wanaotekeleza mashambulizi yao ya kujitoa muhanga dhidi ya nchi yake. Kauli hiyo ya Sharon,imezidi kuweka wazi yale yaliyokuwa yakitangazwa na vyombo vya habari kwamba Israel sasa inakaribia kuondoka katika maeneo inayoyakalia na yale makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi,ili kujiepusha na machafuko zaidi ya Wapalestina. Rais George Bush wa Marekani, amekwisha sema kwamba ujenzi wa ukuta wa zege ngumu na waya wa seng'enge wenye makali mithili ya wembe,ndio kikwazo cha kufikiwa amani ya sasa katika Mashariki ya Kati. Bwana Sharon amekuwa katika shinikizo kutoka Israel kwenyewe akitakiwa kufanya juhudi za kuleta amani.Shutuma hizo hazitoki tu kwa raia wa kawaida, bali hata kwa makamanda wa majeshi yake na wakuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa ndani, Shin Bet. Na hivi leo maofisa wa ngazi za juu wa Palestina na Israel akiwemo mwanawe Sharon,Omri wanakutana mjini London katika semina isiyo rasmi.Pia katika semina hiyo atakuwepo mshauri wa Usalama wa Arafat.Naibu Waziri wa Ulinzi wa Israel,Zeev Boim,amesema mkutano huo ni muhimu kwa vile unakutanisha viongozi wa daraja za juu wa pande zinazohasimiana.
Matangazo