1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nagelsmann aanza kazi kwa mguu mbaya

19 Julai 2021

Vilabu vikuu vya Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga vinapitia kipindi kigumu katika matayarisho yao ya msimu mpya utakaoanza Agosti 13.

Deutschland Fußball FC Bayern Trainer Nagelsmann Flick
Picha: Anke Waelischmiller/Sven Simon/picture alliance

Vilabu hivyo vina hamu sana ya wachezaji wao nyota warudi mazoezini ila wachezaji hao kwa sasa wako likizoni baada ya kushiriki mashindano ya EURO 2020.

Bayern Munich klabu inayoshikilia rekodi ya ubingwa wa ligi ilicheza mechi ya kirafiki mwishoni mwa wiki iliyopita na FC Cologne na chini ya kocha wao mpya Julian Nagelsmann walifungwa magoli 3-2 mbele ya mashabiki elfu sita. Sehemu kubwa ya kikosi cha Bayern ilikuwa wachezaji wa timu ya pili. Wachezaji 13 wa kikosi cha kwanza walioshiriki mashindano ya EURO watarudi mazoezini mwishoni mwa mwezi huu.

Kocha mpya wa Borussia Dortmund Marco Rose naye anakuna kichwa pia tatizo lake kuu likiwa hilo hilo kama la Nagelsmann. Timu yake ilipoteza mechi ya kirafiki 3-1 ilipocheza na VfL Bochum timu iliyopandishwa daraja tu msimu huu. Wakati huo huo Dortmund ambao ni mabingwa wa taji la DFB Pokal, wanatarajiwa kutangaza uhamisho wa nyota wao Jadon Sancho kuelekea Manchester United mara tu ada ya yuro milioni 85 itakapolipwa.

Kocha mwengine anayepitia wakati mgumu ni Adi Hütter wa Borussia Mönchengladbach ambaye timu yake ilicharazwa 3-1 na klabu ya daraja la pili Paderborn katika mechi ya kirafiki. Gladbach pia walitoka sare ya magoli mawili na Viktoria Cologne siku chache kabla mechi hiyo waliyocheza na Paderborn.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW