Nahodha wa Sea-Watch Rackete amuita Salvini "mbaguzi hatari"
6 Julai 2019Matamshi yake , kutokana na mahojiano jana Jumamosi na gazeti la kila siku la Italia La Republica, yameendeleza uhasama na Salvini , ambaye amemueleza Rackete kuwa ni mhalifu pamoja na "Mjerumani mkomunist tajiri ambaye amedekezwa." Katika jibu lake , nahodha huyo anapeleka shauri mahakamani la udhalilishaji.
"Nina wasi wasi juu ya jinsi Matteo Salvini anavyotumia maneno yake , kwa jinsi anavyoeleza mawazo yake ambayo yanakiuka haki za binadamu. Ni mtu hatari lakini wote wenye mawazo ya siasa za kizalendo na siasa kali za mrengo wa kulia wako hivyo, kuanzia chama cha UKIP cha Uingereza hadi chama cha AfD nchini Ujerumani," amesema.
Alipoulizwa iwapo atamwalika Salvini katika meli ya Sea-Watch 3, Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 31 alijibu haitawezekana kwa kiongozi wa Italia wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Ligi kwasababu Sea-watch ina sheria kali: haruhusiwi mbaguzi ndani ya meli."
Rackete aliwachukua wahamiaji 40 kwenda katika kisiwa cha Lampedusa Juni 29, akikaidi amri ya Italia kutoingia katika bandari hiyo. Anaendelea kuwa katika uchunguzi wa kuvunja sheria za uhamiaji za Italia na anatarajiwa kukabiliwa na uchunguzi wa pili siku ya Jumanne.
Wahamiaji
"Katika hali hiyo hiyo ningeweza bila shaka kufanya hivyo hivyo tena, lakini natumai kwamba iwapo kesi kama hii itajitokeza , mara nyingine maafisa wa Italia watachukua hatua haraka na kuzuwia kesi kama hii kutokea," aliliambia gazeti la Republica. Meli ya Rackete , Sea-Watch 3, iliwachukua wahamiaji Juni 12 nje ya pwani ya Libya. Walibakia katika meli yake kwa zaidi ya wiki tatu kwasababu Italia, kwa msisitizo wa Salvini , ilikataa kutoa ruhusa ya kutia nanga meli yake.
Nahodha huyo alisema hatua aliyoichukua ilikuwa muhimu kuleta changamoto ya kisheria kwa sheria ya sasa ya Italia inayopinga wahamiaji ikiongozwa na Salvini. "Baadhi ya nyakati unahitaji kuchukua hatua ya kukaidi sheria na uasi wa kiraia ili kuweza kuimarisha haki za binadamu na kuleta sheria potofu mbele ya sheria," ameongeza.
Akiweka uwiano na raia kutotii sheria chini ya utawala wa wanazi, aliongeza: "Nchini Ujerumani tunafahamu kwamba kulikuwa na nyakati za giza ambapo Wajerumani walifuata sheria na makatazo ambayo hayakuwa mazuri: kwa sababu tu kitu fulani ni sheria haina maana kuwa ni nzuri. Alikiri hata hivyo , "kosa la maamuzi" kwa kugonga boti ya polisi wa forodha wa Italia wakati akiegesha meli yake kisiwani Lampedusa, na kulaumu kuwa alikuwa amechoka. Kikosi hicho cha polisi killikuwa kinajaribu kumzuwia.