1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naibu Mkuu wa Hezbollah: Tuko tayari kwa lolote

30 Septemba 2024

Naibu mkuu wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem ametoa hotuba siku ya Jumatatu na kusema wako tayari kwa lolote katika kukabiliana na Israel.

Lebanon | Naibu mkuu wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem
Naibu mkuu wa Hezbollah Sheikh Naim Qassem akizungumza na wanahabari mjini Lebanon: Julai 2, 2024Picha: Bilal Hussein/AP/picture alliance

Hii ni hotuba ya kwanza tangu shambulio la Israel lilipomuua kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah, ambaye bado haijulikani lini atazikwa, baada ya mwili wake kutambuliwa Jumamosi. Naim Qaseem amesema wako tayari kwa lolote hata kwa mapambano ya ardhini na vikosi vya Israel na kwamba wataendeleza mwongozo ulioachwa na Nassrallah katika vita hivyo.

Kwa upande wake Iran ambayo ndiyo mfadhili mkuu wa Hamas na  Hezbollah ambayo inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa raia wake wanaodai majibu stahiki, imesema inafuatilia kwa karibu yanayoendelea. Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje wa Iran Nasser Kanaani amesema Tehran haitoacha 'vitendo vya uhalifu' vya Israel bila kujibiwa,  akimaanisha mauaji ya viongozi waandamaizi wa Hezbollah nchini Lebanon.

Hassan Nasrallah, Kiongozi wa Hezbollah aliyeuawa hivi karibuni na IsraelPicha: Mohammed Zaatari/AP/picture alliance

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Noel Barrot yuko Beirut akiwa ni mwanadiplomasia wa kwanza wa kigeni wa ngazi za juu kuitembelea Lebanon hivi sasa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi,na amesisitiza kuitaka Israel isitishe mashambulizi hayo.

Soma pia: Hezbollah yaahidi kulipiza kisasi baada ya kuuliwa kiongozi wake

Mbali na miito ya kimataifa ya kutaka kutoutanua mzozo huu wa Mashariki ya Kati, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, ameahidi hivi leo kutoa kifurushi cha msaada cha dharura chenye thamani ya dola milioni 100 kwa Lebanon, huku mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akiitisha mkutano wa dharura wa mawaziri wa umoja huo ili kujadili hali inayozidi kuwa tete nchini Lebanon.

UN: Raia 100,000 wa Lebanon wamekimbilia Syria

Watu zaidi ya 100,000 wamelazimika kuondoka nchini Lebanon na kukimbilia nchini Syria. Hayo ikiwa ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Filippo Grandi ambaye ni Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR. Abbas Sami Dalloul ni raia wa Lebanon aliyekimbilia nchini Syria:

Raia wa Lebanon wakisubiri kuvuka mpaka kuingia SyriaPicha: Hummam Sheikh Ali/Xinhua/picture alliance

"Hatujawahi kushuhudia vita kama hivi, kwa vurugu na uharibifu. Hatukuona uharibifu wa aina hii mwaka 2006 wakati wa mashambulizi ya anga. Kijiji chetu hakikushambuliwa mwaka 2006. Lakini, vita hivi ni vya kikatili kwa vijiji jirani na nyumba zetu. Baada ya siku tatu, watoto walikuwa na hofu.''

Hayo yakiarifiwa, Israel imeendelea kuyalenga maeneo kadhaa ya kundi la Hezbollah ndani ya  Lebanon , huku kukiwa na ripoti kuwa jengo moja la ghorofa limeshambuliwa kwa makombora katikati mwa mji mkuu Beirut. Mamlaka za Lebanon zimesema zaidi ya watu 100 wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Soma pia: Netanyahu aapa kampeni ya kijeshi dhidi ya Hezbollah itaendelea

Katika hatua nyingine, kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas limesema kuwa kiongozi wake nchini Lebanon, Fatah Sharif, ameuawa pamoja na maafisa wengine wawili katika shambulio la anga la Israel kusini mwa Lebanon. Wizara ya Afya ya Lebanon imesema zaidi ya watu 1,000 wameouawa na wengine 6,000 wamejeruhiwa kufuatia wiki mbili za mashambulizi ya Israel.

(Vyanzo: AP, DPAE, Reuters, AFP)