Naibu mkuu wa jeshi la wanamaji la Urusi auawa
3 Julai 2025
Katika taarifa yake, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa Meja Jenerali Mikhail Gudkov, aliyekuwa naibu mkuu wa jeshi la wanamaji, aliuawa jana wakati wa mapigano katika moja ya wilaya za mpakani katika mkoa wa Kursk, unaopakana na Ukraine.
Gudkov, ambaye mnamo Februari alitunukiwa heshima ya juu ya kijeshi katika Ikulu ya Kremlin na Rais Vladimir Putin, anaripotiwa kuwa miongoni mwa maafisa waliouawa katika shambulio la kombora.
Urusi imesema imekamilisha kuudhibiti mkoa wa Luhansk, Ukraine
Kwa mujibu wa mitandao ya kijeshi ya Telegram inayohusiana na majeshi ya Urusi na Ukraine, shambulio hilo lilitokea katika kituo cha kamandi cha Urusi na lilitekelezwa kwa kutumia kombora la HIMARS linalotengenezwa Marekani. Hakukuwa na uthibitisho huru wa madai haya.
Gudkov alishtumiwa na Ukraine kwa madai ya uhalifu wa kivita
Gavana wa Primorsky, Oleg Kozhemyako, amesema Gudkov aliuawa akiwa kazini pamoja na maafisa wengine, na ametuma risala za rambirambi kwa familia zilizoathirika.
Guterres wa Umoja wa Mataifa aahidi kuunga mkono ujenzi mpya wa Ukraine
Hadi sasa, Ukraine haijatoa kauli rasmi kuhusu tukio hilo, lakini hapo awali ilikuwa imewashutumu Gudkov na maafisa wenzake kwa madai ya uhalifu wa kivita madai ambayo yamekuwa yakikanushwa vikali na Urusi.
Denmark yasema ni muhimu kuiimarisha Ukraine na kuiwekea Urusi shinikizo zaidi
Nchini Denmark, waziri mkuu Mette Frederiksen amesema nchi yake itaendelea kuisadia Ukraine kijeshi na kushinikiza vikwazo zaidi dhidi ya Urusi.
Akiwa ameungana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Copenhagen, Frederiksen amesema ni muhimu kuiimarisha Ukraine na kuiwekea Urusi shinikizo zaidi.
Kwa upande wake, Zelensky amesema ziara yao nchini Denmark imeanza kwa mazungumzo muhimu na kusaini makubaliano kadhaa ya ushirikiano.
Zelensky pia amesema kuwa hati iliyotayarishwa kwa ushirikiano kati ya Ukraine na Marekani, itahusisha kampuni kadhaa huku kipaumbele kikuu kikiwa utengenezaji wa droni ya aina mbali mbali.
Zelensky akutana na viongozi mbali mbali wa Umoja wa Ulaya
Zelensky amekutana na Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, katika mji wa Aarhus, akiwa pia na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, pamoja na Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa.
Mazungumzo yao yamejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, misaada ya kibinadamu, na mustakabali wa Ukraine ndani ya Umoja wa Ulaya.
Jeshi la Urusi ladai kuteka kijiji cha Milove mkoani Kharkiv
Jeshi la Urusi limedai leo kuwa limeteka kijiji cha Milove kilichopo katika mkoa wa Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine.
Kijiji hicho sasa kinatajwa kuwa sehemu mpya ya mapigano katika vita vinavyoendelea kati ya nchi hizo jirani.
Ukraine haijatoa tamko rasmi kufuatia madai hayo ya Urusi.
Hata hivyo, katika taarifa ya awali iliyotolewa mapema leo, jeshi la Ukraine lilieleza kuwa vikosi vya Urusi vimekuwa vikijaribu kuvuka mpaka karibu na Milove mara kwa mara, lakini limefanikiwa kuzuia mashambulizi hayo.