Naibu Waziri wa Ukraine asema yawezekana China kusuluhisha
30 Aprili 2023Naibu waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andriy Melnyk amesema mchango wa China katika kusuluhisha vita vya Ukraine unaweza kuwa halisi. Melnyk ameliambia shirika moja la habari la Ujerumani kwamba, licha ya China kuzingatia maslahi yake anaamini kwamba suluhisho la amani na la haki pamoja na kumalizwa mapigano ni mambo yanayokwenda sambamba zaidi na maslahi ya China. Ameeleza kuwa mazungumzo ya hivi karibuni kwa njia ya simu baina ya marais wa Ukraine na China ambayo yalikuwa ya kwanza kufanyika tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, ni hatua kubwa ya kusonga mbele katika kuimarisha uhusiano kati ya China na Ukraine na pia katika kumaliza uvamizi wa Urusi. Melnyk ameeleza kwamba nchi yake inataka Urusi iondoe majeshi yake kwenye maeneo yote ya Ukraine inayoyakalia. Mpango wa China wa kuleta suluhisho la kisiasa hauzingatii kuondolewa kwa majeshi ya Urusi kwenye maeneo ya Ukraine, ikiwa pamoja na rasi ya Crimea iliyotekwa na Urusi mnamo mwaka 2014.