NAIROBI : Burundi yashutumiwa kumfunga mwandishi
20 Septemba 2006Mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za waandishi wa habari yameishutumu Burundi kwa kumfunga kifungo cha miezi mitano mwandishi wa habari anayetuhumiwa kuishutumu serikali ya taifa hilo la Afrika ya Kati.
Serikali ya Rais Piere Nkuruzinza imekuwa ikishutumiwa kwa kuzidi kukandamiza uhuru wa kujieleza ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani.
Aloys Kabura wa shirika la habari la serikali alikamatwa hapo tarehe 31 nwezi wa Mei na kupatikana na hatia ya uasi na kutowa taarifa za kashfa wakati akiwa katika kilabu cha pombe hapo mwezi wa April.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka hukumu hiyo inachukiza na kuchafuwa na kuonyesha kwamba wameazimia kuwakandamiza kwa nguvu zote wale wote wasiofuata msimamo wa chama.
Katika taarifa tafauti kamati ya shirika la Kuwalinda Waandishi yenye makao yake nchini Marekani imesema kufungwa kwa Kabura hakuna msingi wa kisheria na ni sehemu ya kuwazima waandishi wenye sauti za kukosowa.