NAIROBI: Ujumbe wa kundi la LRA utakwenda The Hague, kuhusiana na kesi za wakuu wake za ukiukaji wa haki za binadamu
18 Januari 2007Kundi la wapiganaji wa Lord’s Resistance Army limesema litapeleka ujumbe katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague kushauriana na viongozi wa mashtaka kuhusu kesi za ukiukaji wa haki za binadamu zinazowakabili wakuu wa kundi hilo.
Naibu kiongozi wa kundi hilo, Vincent Otti, amesema mahakama hiyo ilikosea kutoa waranti wa kukamatwa kwao bila kulipa fursa kundi hilo kujieleza.
Hatua hiyo ya Mahakama ya Kimataifa imekuwa kikwazo kikuu cha mashauriano ya amani kati ya serikali na kundi la LRA.
Wakati huo mpatanishi mkuu wa mazungumzo kati ya serikali ya Uganda na kundi la LRA, Riak Machar ambaye ni makamu wa rais wa eneo la kusini la Sudan, amesema mashauriano yatarejewa tena juma lijalo.
Mazungumzo hayo yanafanywa katika mji wa Juba, kusini mwa Sudan.