NAIROBI : Waislamu kushiriki usuluhishi wa Somalia
20 Mei 2007Rais Abdulahi Yusuf wa Somalia ataruhusu wanachama wa kundi la mahkama za Kiislam lililopinduliwa kushiriki katika mkutano ujao wa usuluhishi nchini humo ili mradi wanachaguliwa na koo zao na kukanusha umwagaji damu.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Italia Patrizia Sentinelli akiuelezea uamuzi huo kuwa ni fursa muhimu amesema hapo jana Rais Yusuf inabidi aonyeshe kwa vitendo kile alichokiahidi.
Mkutano wa usuluhishi umepangwa kufanyika tarehe 14 mwezi wa Juni na washiriki watateuliwa na koo zao kwa sababu maamuzi mengi ya kisiasa nchini Somalia hufanywa kwa kuzingatia misingi ya kiukoo.
Sentinelli ambaye ameutembelea mji mkuu wa Mogadishu ulioathirika na vita pia amevitaka vikosi vya Ethiopia kuondoka nchini humo na kutowa nafasi ya kuimarishwa kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini humo.
Serikali ya Italia imekubali kutowa euro milioni 10 kwa kikosi cha Umoja wa Afrika lakini mbali na Uganda mataifa machache ya Afrika yametuma wanajeshi wao kwa kikosi hicho kilichopangwa kuwa na wanajeshi 8,000.