1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI:Wawili wafariki katika mlipuko

11 Juni 2007

Mlipuko umetokea mjini Nairobi leo asubuhi na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi takriban wengine 31.Chanzo cha mlipuko bado hakijajulikana ila kwa mujibu wa Kamishna wa polisi Mohamed Hussein Ali mlipuko ulisababishwa na kitu kilichobebwa na mtu.

Polisi wanaeleza kuwa uchunguzi wa kwanza unabaini kuwa mtu mmoja alijaribu kuingia mkahawa mmoja nao walinzi walijaribu kumzuia kuingia kwani alikuwa na mavazi ya kutatanisha.Haijulikani iwapo mtu huyo alihusika na mlipuko huo.Mlipuko huo umetokea kwenye duka moja katika Hoteli ya Ambassadeur.Hoteli yenyewe haikuathirika.

Mlipuko huo umesababisha thamani ya shilingi ya Kenya kushuka kutoka 66.40 hadi 67.10 kwa kila dola moja ya Marekani.

Yote haya yanatokea wiki kadhaa baada ya ghasia zilizosababishwa na kundi lililopigwa marufuku la Mungiki kuchinja na kuuwa watu.Zaidi ya watu 30 waliuliwa na polisi wiki jana walipokuwa wakiwasaka wafuasi wa Mungiki katika mtaa wa mabanda wa Mathare.Shambulio jengine la bomu lilitokea mwaka 98 kwenye ubalozi wa Marekani na kusababisha vifo vya watu 200.Tukio la leo limetokea karibu na eneo hilo la ubalozi.Bomu jengine liliripuka mwaka 2002 katika Hoteli ya Waisraeli ya Paradise eneo la Kikambala katika pwani ya Kenya.