1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Najib Mikati apata wingi kuteuliwa waziri mkuu mpya Lebanon

26 Julai 2021

Mfanyabiashara wa Lebanon na waziri mkuu wa zamani Najib Mikati amepata kura za kutosha katika mashauriano ya bungeni ili kuteuliwa kuunda serikali tena baada ya kuungwa mkono na vyama vikuu.

Najib Mikati
Picha: Reuters

Kuteuliwa kwake kuwa waziri mkuu kumekuja baada ya mwanasiasa veterani wa madhehebu ya Kisunni Saad al-Hariri kuachana na juhudi za kuunda serikali mapema mwezi huu, baada ya miezi tisa ya mkwamo na rais Michel Aoun, mkuu wa nchi wa madhehebu ya Kikristo ya Maronite.

Masuala yaliosababisa mkwamo kwa juhudi za Hariri kuunda baraza, ikiwemo takwa la Aoun la kuwa kura ya turufu serikalini, yumkini yataendelea kutia ugumu wa jukumu hilo.

Soma pia: Lebanon huenda ikatumbukia kwenye mzozo zaidi

Malumbano ya kisiasa yameiacha Lebanon bila serikali thabiti wakati ambapo nchi hiyo ikizidi kudidimia katika mzozo wa kiuchumi na kifedha.

Waziri Mkuu Hassan Diab, ambaye baraza lake lilijiuzulu mwezi Agosti kufuatia mlipuko katika bandari ya Beirut, ameendelea kushika wadhifa wa waziri mkuu wa mpito hadi serikali mpya itakapoundwa.

Mikati ambaye amekuwa waziri mkuu mara mbili akiwa madarakani kwa mara ya mwisho mwaka 2014, alipata wingi wa wazi wa kura 72 kutoka kwa wabunge waliokaa kwa ajili ya mashauriano na rais siku ya Jumatano.

Rais wa Lebanon Michel Aoun, kushoto, akikutana na waziri mkuu wa zamani Najib Mikati katika ikulu ya rais, iliyopo Baabda, mashariki mwa Beirut, Jumatatu, Julai 26,2021. Mikati amepata uungwaji mkono wa kutosha wa wabunge kuunda serikali.Picha: Dalati Nohra/Lebanese Official Government/AP Photo/picture alliance

Mgombea wa muafaka

Aliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa waziri mkuu wa mpito Aprili 2005, wakati mzozo kuhusu mauaji ya Rafiki Hariri ulipoilazimu Syria kuondoa wanajeshi wake kutoka Lebanon.

Mikati alihudumu kwa miezi mitatu hadi uchaguzi ulioupa ushindi muungano wa vyama vya Kisunni, Druze na Wakristu, ukiogozwa na matoto wa Hariri, Saad.

Mikati mwenye umri wa miaka 65, aliteuliwa tena kuwa waziri mkuu Juni 2011, na kujiuzulu Mei 2013 na kusalia kama waziri mkuu wa muda hadi Februari 2014.

Soma pia: Waziri Mkuu Mteule wa Lebanon Mustapha Adib ajiuzulu

Msomi huyo wa chuo kikuu cha Havard alianza kujenga biashara yake ya Investcom katikati mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon. Aliuza hisa zake katika kampuni ya MTN ya Afrika Kusini kwa kias cha dola bilioni 5.5 mwaka 2006.

Mwaka 2007, alianzisha kampuni ya M1, ambayo inawekeza katika maeneo tofautitofauti. Mwezi huu, kampuni ya mawasiliano ya Norway, telenor, iliuza operesheni zake za nchini Myanmar kwa kundi la M1 kwa kiasi cha dola milioni 105.

Mikati pia alihudumu kama waziri wa ujenzi na usafiri katika mabaraza matatu kati ya 1998 na 2004.

Tahadhari kuhusu mdororo wa kiuchumi Lebanon

01:03

This browser does not support the video element.

Tofauti na viongozi wengi wa Lebanon, Mikati hatokei katika mmoja ya himaya zake nyingi za kisiasa, hali inayomfanya kuwa mgombea muafaka wa nafasi ya waziri mkuu.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW