1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Najib Razak wa Malaysia kukata rufaa hukumu ya ufisadi

28 Julai 2020

Waziri Mkuu wa zamani wa Malaysia, Najib Razak, atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu mjini Kuala Lumpur kumtia hatiani kwa mashitaka ya ufisadi dhidi yake na kumhukumu kifungo cha miaka 12.

Malaysia | Ex-Premier Najib Razak festgenommen
Picha: Reuters/L. S. Sin

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la mahakama mjini Kuala Lumpur mchana wa Jumanne (29 Julai), Najib alisema kuwa mashitaka dhidi yake yalikuwa ya kisiasa na kwamba hahusiki na kadhiya hiyo ya ubadhirifu wa kiasi cha mabilioni ya dola yaliyotoweka kwenye mfuko wa maendeleo wa serikali, maarufu kama kashfa ya 1MDB:

"Kama ilivyo kawaida, mtu hutegemea kheri lakini hujiandaa kwa shari. Na huu si mwisho wa dunia. Bado kuna nafasi ya kuukatia rufaa uamuzi huu, nasi tutaelekea huko na naamini tutafanikiwa. Kwa wafuasi wangu, natarajia wataendelea kuniunga mkono na kuniamini na kuamini mapambano yetu na kutovunjika moyo," alisema.

Awali Jaji Muhammad Nazlan Ghazali wa Mahakama Kuu mjini Kuala Lumpur alisema ameridhika na hoja zilizowasilishwa na upande wa mashitaka dhidi ya Najib, ikiwa ni sehemu ya mlolongo wa kesi kadhaa za ufisadi dhidi yake.

Ndani ya chumba cha mahakama, Najib, ambaye serikali yake iliporomaka miaka miwili iliyopita kutokana na kashfa hiyo ya kukwapuwa mabilioni ya dola kutoka hazina ya taifa, alionekana mtulivu. Alishika msahafu kizimbani akiapa kwamba hana hatia ya kosa lolote. 

Hukumu ya miaka 72?

Jaji anasema Najib ana hatia kwenye mashitaka yote saba aliyoshitakiwa.Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Thain

Jaji Ghazali alisema anamuhukumu Najib kifungo cha miaka 12 jela kwa shitaka moja la kutumia vibaya madaraka yake, miaka 10 kwa kila kosa kati ya matatu ya kuvunja uaminifu, na miaka mingine 10 kwa kila kosa kati ya matatu ya kutakatisha fedha.

Hata hivyo, Jaji huyo aliamuru hukumu hizo zote kuchanganywa pamoja, ikimaanisha kuwa Najib atatumikia kifungo cha miaka 12 tu.

Jaji huyo, ambaye pia alimtaka Najib kulipa faini ya dola milioni 49.4, aliruhusu kusitishwa kwanza kutekelezwa kwa hukumu yake hadi hapo rufaa ya mtuhumiwa itakapomaliza kusikilizwa. 

Hukumu hii ya kesi moja kati ya tano za ufisadi imetolewa ikiwa ni miezi mitano tu tangu chama cha Najib, Malay, kurejea serikalini kikiwa mshirika mkuu kwenye muungano wa vyama tawala, uliochukuwa madaraka baada ya serikali ya kimageuzi iliyoingia madarakani mwaka 2018 kuporomoka. 

Wachambuzi wanasema hukumu ya leo itaimarisha hoja ya waendesha mashitaka kwenye kesi nyengine zinazomkabili Najib na inatoa ujumbe kwa wafanyabiashara wakubwa nchini Malaysia kwamba sasa muhimili wa mahakama una nguvu za kutosha kushughulikia uhalifu wa kifedha wa kimataifa.

Hata hivyo, wako wanaokhofia kwamba hukumu hii itapinduliwa kwenye mahakama ya rufaa, kwani chama cha Najib kipo madarakani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW