1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Namibia baada ya kifo cha Rais Geingob

Hawa Bihoga
12 Februari 2024

Namibia imekamilisha makabidhiano ya madaraka baada ya kifo cha Rais Hage Geingob aliyefariki baada ya kuugua saratani kwa muda mfupi. Lakini mwelekeo wa kisiasa katika taifa hilo ni upi?

Rais Nangolo Mbumba wa Namibia.
Rais mpya wa Namibia, Nangolo Mbumba, akila kiapo kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha Rais Hage Geingob.Picha: Sharon Kavhu/Xinhua/picture alliance

Rais wa mpito, Nangolo Mbumba, alichukua usukani, akisema hana mpango wa kugombea uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba.

"Sitakuwepo kwa ajili ya uchaguzi. Kwa hivyo, msiwe na shaka," Mbumba alisema katika hafla ya kuapishwa kwake siku ambayo mtangulizi wake, Hage, alifariki.

Maamuzi ya Mbumba ni ya nadra miongoni mwa viongozi wa Afrika, ambao mara nyingi huwa na tabia ya kuchukuwa fursa yoyote waliyonayo ya kusalia madarakani.

Soma: Mgombea binafsi Namibia awasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi

Wakati akitoa heshima zake kwa mtangulizi wake alisema taifa la Namibia linasalia na utulivu kutokana na uongozi wa Rais Geingob, ambaye alikuwa ni miongoni mwa watengenezaji wakuu wa katiba.

Marehemu Hage Geingob, rais wa zamani wa Namibia.Picha: Phill Magakoe/AFP/Getty Images

Kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, uteuzi wa Mbumba kama rais wa mpito halikuwa jambo la kushangaza.

Wanasema Mbumba alikuwa ni chaguo bora kwa ajili ya kuendeleza yale yaliyosalia katika ofisi ya rais. Mbumba alikuwa naibu wa Geingob tangu mwaka wa 2018.

Wakati Geingob alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza 2015, tayari Mbumba alishakuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa kipindi kirefu - kuanzia 1990 hadi 2002 na akarejea tena kwa muda mfupi mwaka 2012 hadi 2015. 

Geingob alikufa akiwa umashuhuri umeshuka

Hata hivyo, kulingana na matokeo ya kura ya maoni, umaarufu wa Geingob ulikuwa umeshuka wakati anafariki dunia, kwani katika uchaguzi wa 2014 alipata ushindi wa kishindo kwa asilimia 87 ya kura, lakini miaka mitano baadaye kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 56.

Namibia wapiga kura

01:11

This browser does not support the video element.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia katika awamu ya kwanza ya Geingob iliambatana na uchumi uliozorota, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira na umasikini. Chama chake pia kilikabiliwa na kashfa kadhaa za ufisadi wakati akiwa madarakani.

Mbumba alimteua Netumbo Nandi-Ndaitwah ambaye alikuwa naibu waziri mkuu wa zamani na mgombea urais kwa tiketi ya chama tawala cha South West Africa People's Organization (SWAPO) kama makamu wa rais.

Iwapo atachaguliwa mwezi Novemba, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 71 atakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Namibia.

Wachambuzi wanasema kuwa naye kama mgombea urais ni hatua ya kimkakati inayohakikisha utulivu ndani ya chama, ambacho kwa sasa kinajikuta hakina kiongozi.

Inatarajiwa kuwa SWAPO itafanya mkutano usio wa kawaida ndani ya siku 90 kumchagua kada mpya ili kuchukua uongozi wa chama baada ya mwendazake, Rais Geingob.

Wakati Nandi-Ndaitwah anaonekana kuwa mgombeaji wa nafasi hii, Mbumba pia ana nafasi ya kuwa kiongozi ajaye wa chama.

Upinzani hautafaidika na kifo cha Geingob

Hata hivyo, hiyo haitabadilisha mwelekeo wa siasa za chama kabla ya uchaguzi wa baadaye mwaka huu.

Rais mpya wa Namibia, Nangolo Mbumba (kushoto), na makamu wake, Netumbo Nandi-Ndaitwa.Picha: Ester Mbathera/AP/picture alliance

"Natarajia SWAPO ibaki katika mwelekeo wa kumbakisha Nandi-Ndaitwah kama mgombea wa chama," anasema mmoja wa wachambuzi hao, Andreas, ambaye anaongeza kuwa hatua hiyo itajenga dhana ya wapigakura kwamba kuna utulivu katika chama.

Soma zaidi: Wananchi wa Namibia wapiga kura

Alionya kuwa mabadiliko yoyote ya dakika za mwisho ya wagombea yanaweza kuonesha chama hakina utulivu mbele ya wapiga kura, huku ufafanuzi wake ukigeukia upande wa pili ya sarafu akisema kuonesha nguvu na umoja pia kunaweza kutoa pigo kwa matumaini yoyote ya vyama vya upinzani kunufaika na kifo cha Geingob.

Lakini mambo yanatazamwa tofauti na Henning Melber, mfuatiliaji wa muda mrefu wa siasa za Namibia.

Aliiambia DW kuwa chama tawala, SWAPO, kinakaribia kupoteza idadi kubwa ya watu wake kuliko hapo awali kutokana na kukwama katika fikra za ukombozi.

Lakini Melber anasema kuna karata moja iliyosalia: nayo ni mgawanyiko miongoni mwa wapinzani Namibia.