Namibia yafanya kumbukumbu ya kwanza ya mauaji ya kimbari
29 Mei 2025
Namibia iliadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari siku ya Jumatano, kwa kuwakumbuka wahanga wa utawala wa ukoloni wa Kijerumani katika hafla maalum iliyohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye bustani ya bunge mjini Windhoek. Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah aliielezea siku hiyo kuwa ya majonzi ya pamoja, ya kuwakumbuka wale waliouawa, pamoja na kuenzi kumbukumbu ya kihistoria iliyowaacha wananchi na maumivu ya kihisia, kiuchumi na kitamaduni ambayo bado yanaonekana hadi leo.
Siku hiyo ya kitaifa inalenga kukumbuka mauaji ya kimbari ya maelfu ya watu wa jamii ya Herero na Nama kati ya mwaka 1904 na 1908, kipindi ambacho Namibia—iliyokuwa ikijulikana kama Afrika ya Kusini Magharibi—ilikuwa koloni la Ujerumani. Wanahistoria wanakadiria kuwa karibu watu 65,000 kati ya 80,000 wa jamii ya Herero na nusu ya watu 20,000 wa jamii ya Nama waliuawa. Mauaji haya yanachukuliwa na wataalamu wengi wa historia kama ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20.
Kumbukumbu kuwa ya kila mwaka
Serikali ya Namibia imetangaza kuwa kumbukumbu hii itaadhimishwa kila mwaka kama siku ya umoja wa kitaifa na tafakari ya pamoja juu ya historia ya taifa hilo. Viongozi wa kijamii na wawakilishi wa waathirika wamesema hatua hiyo inatuma ujumbe mzito kwa serikali ya Ujerumani, wakitaka hatua zaidi za kutambua na kurekebisha madhila ya kihistoria.
Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Reem Alabali-Radovan, aliuelezea ukatili wa wakati huo kuwa ni "jinai isiyovumilika" ambayo ni sehemu ya historia ya taifa la Ujerumani. Alisisitiza kuwa ni wajibu wa serikali yake kukabiliana na historia hiyo kwa uwazi, na kuchukua hatua za kupunguza athari za kihistoria kwa watu wa Namibia.
Serikali za Ujerumani na Namibia zimekuwa zikijadiliana kwa muda mrefu juu ya makubaliano ya maridhiano, ambayo yanajumuisha msaada wa maendeleo wenye thamani ya euro bilioni 1.1 kutoka Ujerumani. Hata hivyo, utekelezaji wa makubaliano hayo umecheleweshwa kutokana na Ujerumani kusisitiza kujadiliana na serikali ya Namibia badala ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na jamii za waathirika, jambo ambalo limeibua ukosoaji kutoka kwa baadhi ya wawakilishi wa Herero na Nama.