1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Namna dhahabu ya afrika inavyotoroshwa kila mwaka

25 Aprili 2019

Madini ya dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya dola yanatoroshwa kutoka Afrika kila mwaka kwa kupitia nchi za mashariki ya Kati na kuuzwa kwenye masoko ya Ulaya na Marekani.

USA Miamis Goldhandel
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/Miami Herald

Kwa mujibu wa uchunguzi  uliofanywa na shirika la habari la Reuters, Umoja wa Falme za Kiarabu uliingiza katika nchi zao dhahabu yenye thamani ya dola bilioni 15.1 kutoka Afrika mnamo mwaka 2016 pekee. 

Kulingana na uchunguzi wa shirika hilo la Reuters kuanzia mwaka 2006  hadi mwaka 2016 nchi hiyo ya kiarabu iliingiza tani 446  za dhahabu kutoka nchi za Afrika. Kiwango kikubwa cha dhahabu hiyo hakikuorodheshwa katika bidhaa zinazouzwa nje na nchi za Afrika. Watalamu waliohojiwa na shirika hilo wamesema kiasi kikubwa cha madini hayo kinatolewa nje ya Afrika bila ya kutozwa kodi na  nchi zinazozalisha madini hayo hazipati kitu.

Kampuni za madini za barani Afrika zimeliambia shirika la Reuters kuwa kampuni hizo haziuzi dhahabu kwa Umoja wa Falme za kiarabu.Tamko hilo linathibitisha kwamba dhahabu hiyo inaingia katika nchi hiyo kwa njia ambayo si rasmi.

Mwanamke kutoka Kakamega Kenya akiwa ameshikilia kipande cha dhahabuPicha: picture-alliance/abaca/AA/R. Canik

Serikali za Ghana,Tanzania na Zambia zimelalamika kwamba  dhahabu ya nchi hizo inatoroshwa kwa kiwango kikubwa na magenge ya wahalifu na aghalabu katika muktadha wa madhara makubwa kwa mazingira na afya ya binadamu.

Shughuli za kuchimba dhahabu ambazo hapo awali zilikuwa zinafanywa na wafanyabiashara wadogo katika nchi hizo za Afrika sasa imechukuliwa na makampuni makubwa kutoka nje  ya Afrika.Hayo alisema hivi karibuni rais wa Ghana Nana Akufo.

Mfano ,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni mzalishaji mkubwa  wa Dhahabu lakini nchi hiyo inaambulia kiasi kidogo cha fedha zinazotokana na mauzo ya bidhaa hiyo nje ya nchi.Dhahabu ya nchi  hiyo inaporwa na watu kutoka nchi jirani.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kwamba kituo kikuu ambapo dhahabu ya Afrika inateremshwa ni Umoja wa Falme za kiarabu UAE.Lakini mnamo mwaka  2015 China iliingiza  nchini, kiwango kikubwa cha dhahabu kutoka Afrika kuliko nchi  hiyo  ya kiarabu.Hata hivyo mnamo  mwaka 2016  nchi  hiyo  ya  kiarabu  iliingiza dhahabu kutokaa Afrika yenye  thamani ya dola bilioni 7.4. Mshauri mwandamizi wa maendeleo ya viwanda wa Umoja wa  Afrika, Frank Mugyenyia amesema kiwango kikubwa cha dhahabu kinauzwa nje ya Afrika bila ya daftari.

Soma zaidi..

Mahitaji makubwa ya dhahabu katika kipindi cha mwongo uliopita pia yameongeza madhara katika mazingira.  Vifaa vinavyotumiwa  na  wachimbaji wa dhahabu vinaongeza uzalishaji lakini katika  mchakato wa kuchimba dhahabu hiyo maji ya sumu yanaingia  kwenye mito na kuathiri afya za watu wanaotumia maji hayo. Maji hayo ya sumu yanasababisha maradhi kwenye ini,  mafigo,bandama na mapafu. Serikali za Afrika zinajaribu kutafuta njia ya kuisimamia sekta hiyo kwa sababu inawaingizia wananchi wengi mapato.

Wachimba madini wadogo wadogo huko nchini NigerPicha: Getty Images/AFP/C. Aldehuela

Nchini Tanzania taarifa ya bunge imeonyesha kwamba asilimia 90 ya dhahabu inayozalishwa nje ya taratibu rasmi, inatoroshwa nje ya nchi. Sasa serikali inaitaka benki kuu ya nchi hiyo inunue dhahabu kutoka kwa wachimbaji. Serikali ya Tanzania inapanga kuanzisha vituo rasmi vya biashara ya dhahabu. Bei ya dhahabu sasa inafikia dola 40,000 kwa kilo. Kadri inavyotoroshwa na kuuzwa nje, nchi za Afrika zinaingia hasara ya mabilioni kila mwaka, kwa mujibu wa uchunguzi wa shirika la Reuters.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW