Nangira kufanya mageuzi ya huduma ya afya vijijini
20 Agosti 2018Katika jamii nyingi za Kiafrika, watoto hupewa jina kutokana na hali, mazingira au msimu alimozaliwa au kwa ajili ya kumwenzi mzazi alietangulia dunia kama hatua njia ya kumkumbuka na kuendeleza jina la ukoo. Katika jamii ya Basamia na Bagwe nchini Uganda na hata ndugu zao wa jamii za Babukusu na Luhya nchini Kenya, mtoto aliyezaliwa njiani pengine mamake akielekea kituo cha afya au kwingineko huitwa Wangira akiwa mvulana na akiwa msichana huitwa Nangira. Hii ina maana kuwa tangu siku yake ya kwanza duniani, Betty Nangira alikabiliwa na tatizo la upatikanaji wa huduma za afya.
"Nilizaliwa njiani mamangu alipokuwa akielekea kwenye kituo cha afya. Alipokuwa akitembea alilazimika kujifungulia njiani na ndiyo maana aliniita Nangila” Nangira anafafanua kwa nini aliitwa jina hilo.
Hii ndiyo moja wapo ya sababu zilizompelekea Nangira kujihusisha na utafiti kuhusu upatikanaji wa huduma za afya, akiangazia hasa sera zinazotakiwa kuzingatiwa katika utoaji wa huduma hiyo vijijini. Licha ya kuwepo kwa sera inayoelezea kuwa matibabu katika vituo vya afya vya serikali ni bure, ukweli ni kwamba wagonjwa hutakiwa kujinunulia vifaa na dawa wanazoshauriwa na madaktari kutumia. Hali hio inapelekea familia kutumia kiasi kikubwa cha pesa kwa matibabu, na hivyo kuwatumbukiza zaidi katika umasikini.
Kinachoshangaza anasema Nangira ni kwamba viongozi wa ngazi za mashinani hawajawasilisha hoja hiyo kwa serikali kuu. Hizo ni miongoni mwa changamoto ambazo Nangira anataka kuvitafutia suhulu kupitia utafiti wake. "Unakuta kwamba mama anayetokea familia masikini isiyo na uwezo kifedha hawezi kujinunulia vifaa hivyo,” anaeleza Nangira.
Homu ya wagonjwa
Kwa upande mwingine ni wazi kuwa baadhi ya wagonjwa wanaogopa kwenda kwenye vituo vya afya kwa hofu ya kusemwa vibaya na wahudumu wa afya kutokana na jinsi walivyo vaa. Hata kama vituo hivyo viko karibu na wagonjwa masuala kama hayo huwatia fedheha wagonjwa, anaongeza Nangira.
Migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi wa afya wakidai nyongeza ya mishahara pamoja na maslahi bora ya kufanya kazi ni dhihirisho kuwa wengi wao hawafurahii mazingira ya kazi. Baadhi yao huamua kufungua kiliniki na maduka ya dawa binafsi huku wakidokoa dawa za serikali na kuwauzia wagonjwa.
Kwa mujibu wa utafiti wake wa awali, Nangira amegundua masuala kadhaa ambayo atayachunguza kwa kina kabla ya kufikia hatua ya kutoa mapendekezo. Ana mtazamo kuwa serikali haijaipa sekta ya afya ufadhili unoastahili ilhali afya ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Badala yake masuala ya usalama ndiyo yamezingatiwa zaidi kuliko afya ya raia.
Mara nyingi mashehena ya dawa zilizopitwa na muda wake huchomwa moto nchini Uganda. Hii imewapelekea wananchi wengi kuhoji kama kweli kuna mkakati maalumu wa ufuatiliaji kuhusu mahitaji ya wagonjwa. Kwa upande mwingine utawasikia watu wakidai eti vituo vya afya vya serikali havina dawa. Nangira anaamini utafiti wake utajitokeza na ufumbuzi kuhusu suala hilo, huku akiikumbusha mamlaka husika ya afya kuwa hata huo uchomaji wa shehena za dawa hugharimu kiasi kikubwa cha fedha kwa kuwa ni mchakato unaotakiwa kufanywa kwa namna maalumu iliyo salama kwa afya ya jamii.
Nangira anaongeza kuwa "kwa mujibu wa utafiti na taarifa mbalimbali za vyombo vyombo vya habari, tunafahamishwa kuwa wengi wa wafanyakazi wa afya hawana motisha kabisa kwani hulipwa mishahara duni sana.”
Ugumu wa kupata taarifa
Nangira anafahamu kuwa suala analofuatilia kwa sehemu ni la kisiasa na kwa namna hiyo hatopata taarifa anazohitaji kwa wepesi kutoka kwa wasimamizi wa vituo vya afya. Wengi watajaribu kukwepa maswali yake pamoja na kuahirisha miadi ya kukutana nao.
Kwa upande mwingine kuna waganga na wakunga wa kienyeji wanaotumia dawa za asli za mitishamba katika matibabu. Hadi sasa watu hao ni muhimu katika suala zima la afya ya jamii licha ya kuwa serikali inapinga vikali shughuli zao kwa kuziharamisha. Nangira angependa kuchunguza mchango wanaotoa watu hao kwa afya ya jamii za vijijini. Lakini anahisi kwamba itakuwa kazi kubwa kuwashawishi hadi wakubali kutoa kauli zao. Ama baada ya kukamilisha na kuwasilisha kazi yake ya utafiti, Nangira anataraji kwamba mapendekezo yake yataleta mageuzi makubwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya vijijini iwapo yatatekelezwa na taasisi husika.
Betty Nangira anaendesha utafiti huu kwa ajili ya kutunukiwa shahada ya uzamifu sambamba na kuchangia maarifa yanayolenga kuwepo kwa sera thabiti za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya vijijini nchini Uganda na nchi zingine za Afrika. Shughuli zake zinafadhiliwa na Lisa Maskell taasisi ya Kijerumani ya Gerda Henkel.
Mwandishi: Lubega, Emmanuel
Mhariri: Buwayhid, Yusra