1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Nani atakuwa Rais mpya wa Nigeria?

25 Februari 2023

Mamilioni ya raia wa Nigeria wamepiga kura leo Jumamosi kumchagua rais mpya na Bunge jipya.

Nigeria | Wahltag
Picha: Uwais Abubakar Idris/DW

Wakiwa na shauku ya mabadiliko baada ya miaka kumi ya rais Muhamadu Buhari, mamia kwa maelfu ya raia wa taifa hilo wameteremka katika vituo vya kupigia kura tangu mapema asubuhi kuamua nani atakuwa kiongozi ajaye.

Matumaini ya wengi ni kwamba kiongozi mpya atapatikana katika mchakato wa uchaguzi ulio wa huru na haki na atakuwa na jukumu la kupambana na ukosefu wa usalama kwenye taifa hilo na hali ngumu ya uchumi.

Tangu kwenye mitaa ya familia za kipato cha chini kwenye mji wa kibiashara wa Lagos hadi kwenye viunga vya nusu jangwa huko kwenye mji wa pili kwa ukubwa wa Kano ulio kaskazini magharibi mwa Nigeria, raia wa taifa hilo wameshiriki uchaguzi huo ulio na ushindani mkubwa.

Wagombea watatu kati ya 18 wanaowania kiti cha rais ndiyo wanapigiwa upatu kuwa wanaweza kumrithi Buhari anayehitimisha kipindi chake cha pili.

Shauku ya kutimiza haki ya kikatiba ni kubwa 

Kwenye mji wa Lagos muda mrefu wa kusubiri kupiga kura pamoja na matatizo kadhaa ya kiufundi kwenye mifumo ya elektroniki ya kuwatambua wapiga kura viliwafadhaisha baadhi ya raia waliokwenda vituoni.

Licha ya changamoto kwenye mifumo ya kutambua wapigakura, raia wa Nigeria wengi wamesubiri vituoni kutimiza haki hiyo.Picha: Uwais Abubakar Idris/DW

Hali hiyo imeripotiwa pia huko Kano na kwenye mji wa ulio kitovu cha uzalishaji mafuta wa Port Harcourt. Hata hivyo wengi hawakukata tamaa wakisema uchaguzi huo ni muhimu na hawawezi kuacha kupiga kura.

Sehemu kubwa ya mitaa haikuwa kabisa na magari mjini Lagos na wengi ya watu walionekana viwanjani au wakipiga soga mitaani.

Ulinzi umeimarishwa sana nchini humo huku wanajeshi na polisi wakishika doria kutokea kwenye vituo vya usalama na ukaguzi vilivyotawanywa kwenye miji mbalimbali nchini Nigeria.

"Nina furaha sana kutimiza haki yangu ya kuchagua viongozi wetu. Tumetesa vya kutosha kwenye taifa hili” amekaririwa Josephine Patrick, mbunifu wa mavazi mwenye umri wa miaka 31 aliyepiga kura mjini Lagos.

Ameongeza kusema ana matumaini uchaguzi huo utaleta mabadiliko wanayotaka Wanigeria kwa udi na uvumba.

Ni mgombea wa chama tawala au yule wa upinzani?

Tume huru ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema haifahamu hasa ni wakati gani matokeo yatakuwa tayari lakini wameahidi kulifanya zoezi la kuhesabu kura kwa haraka.

Bola Tinubu wa chama tawala cha APC (kushoto) na Atiku Abubakar wa chama cha upinzani cha

Mbali ya uchaguzi wa bunge jipya Wanigeria wengi wanatupia macho kinyang´anyiro cha urais.

Wafuasi wa chama tawala cha All Progressives Congress au APC wanamuona mgombea wao, Bola Tinubu, mwenye umri wa miaka 70 kuwa chaguo lisilo na mbadala na aliyebeba matumaini ya mageuzi.

"Anao uzoefu” anasema Tairu Aramide, mwenye umri wa miaka 57, anayefanya kazi ya upishi mtaani na ambaye amempigia kura Tinubu. Mama huyo anasema usiku wa kuamkia leo amelala karibu na kituo cha kupigia kura kwa sababu anaishi mbali.    

Anampigia upatu mgombea wake akisema anayo rikodi nzuri ya utumishi ikiwemo "alipokuwa gavana wa Lagos amefanya mengi na ataenda kuunda nafasi nyingi za kazi na kuimarisha miundombinu muhimu ambayo taifa hili inahitaji sana.”

Waungaji mkono wa mgombea mwengine kinara Atiku Abubakar mwenye umri wa miaka 76, na anayeongoza kambi ya upinzani kupitia chama cha  Peoples Democratic Party au PDP, wanasema ataleta uzoefu mkubwa serikali kutokana na tajriba aliyojizolea alipokuwa Makamu wa rais.

Lakini huenda watabadili karata za vyama vikubwa?

Peter Obi wa chama cha La our Picha: Katrin Gänsler/DW

Hata hivyo yuko mgombea mwengine Peter Obi, anayevutia hisia na uungaji mkono wa wengi. Vijana wanamtazama kama chachu ya mabadiliko ya kweli. Mwanasiasa huyo anatokea chama cha Labour.

"Obi ndiyo chagua la Nigeria. Tulitaraji makubwa kutoka kwa viongozi waliotangulia lakini tunaona Obi ndiye mgombea mwenye uwezo wa kufanya mabadiliko ya kweli” anasema Stephen Franklin anayeishi mjini Port Harcourt.

Baada ya tambo za miezi chungunzima, raia wa taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu na uchumi mkubwa barani Afrika watatambua katika muda usio mrefu nani atarithi mikoba ya Buhari na iwapo atamudu kutimiza matarajio yao.

Walau kwa sasa wengi wanakaa kwa shauku majumbani au mitaani nchini Nigeria wakisubiri matokeo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW