1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani wataunda serikali ya mseto na Merkel?

20 Septemba 2017

Vyama viwili vinavyotajwa huenda vikaunda serikali na muungano wa Merkel CDU/CSU vina uhasama wa tangu jadi-je itawezekana kupatikana kile kinachoitwa bendera ya Jamaica?

Deutschland Christian Lindner und Cem Özdemir bei ZDF-Gesprächsrunde Maybritt Illner (2013)
Picha: picture-alliance/dpa/K. Schindler

Chama cha Kijani na kile cha wanaopendelea masuala ya biashara cha Free Democrats tangu jadi ni vyama ambavyo vimekuwa mahasimu wakubwa katika siasa za Ujerumani. Lakini je inawezekana vyama hivi viwili vidogo kuweka pembeni tafauti zao kwa ajili ya kuunda serikali ya muungano na wahafidhina na kugawana madaraka?

Ikiwa uchunguzi wa maoni utakuwa sawa basi uchaguzi wa Ujerumani Septemba 24 utahitaji kujitolewa kwa kiasi kikubwa. Endapo serikali ya mseto wa vyama vikuu ya sasa kati ya vyama vya kihafidhina na Social Demokrat ambacho kwa kiasi kikubwa kinaangaliwa kama chama kilichopwaya haitoendelea,  basi vyama vinavyoonekana wazi kwamba vitapata wingi kwa sasa inaoesha ndivvyo vitakavyounda muungano wa pande tatu ambavyo ni kati ya wahafidhina, Walinzi wa Mazingira  na FDP.

Muungano ambao kwa Wajerumani umepewa jina la ''mseto wa Jamaica'' kwa sababu ya rangi ya vyama hivyo vitatu zinaoana na rangi ya bendera ya Jamaica. Ikitokea hali hiyo itamaanisha kitu kipya na tafauti kabisa katika siasa za Ujerumani.

Picha: Imago/R. Traut

Lakini kitu ambacho kinafahamika Ujerumani ni kwamba vyama hivi viwili wanamazingira na FDP hawapikwi chungu kimoja. Jurgen Dittberner ambaye ni profesa wa masuala ya siasa ambaye anamaingiliano na chama cha FDP ameliambia shirika la DW kwamba vyama hivi viwili vyote vinagombea eneo sawa. Na kama ilivyo mara nyingi mafahali wawili hawakai zizi moja.

Licha ya kuwepo juhudi hivi karibuni za kumaliza uhasama huo vyama hivi viwili Waliberali kama wanavyoitwa FDP  na wanamazingira  wamekuwa na utamaduni wa kutopendana na mara nyingine uhasama huo hujitokeza kwa aina yake. Kwa mfano, Chama cha Kijani kimeiga na kutengeneza  mabango ya kampeini ya chama cha FDP na kumuonesha mgombea wa juu wa chama hicho cha FDP, Christian Lindner, kama kijana anayeendesha gari aina ya Porsche huku nako chama hicho cha kiliberali cha FDP kikikishambulia chama cha kijani kwa kukionesha kuwa ni chama kinacho juwa tu mambo yanayohusiana na miti na misitu. Kwa maana hii washwahili tabia haina dawa na kuchukiana baina ya vyama hivi ni desturi ya tangu jadi.

Wagombea wa chama cha Kijani na CSU wakimtazama mgombea wa FDP akijipiga picha ya SelfiePicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Historia ya uhasama kati ya vyama hivi viwili inatokea mbali na uhasama huu unahusiana zaidi na mambo yaliyopita muda mrefu kuliko sera za sasa. Chama cha FDP kiliasisiwa 1948 na chama hicho kimeanzia katika serikali ya shirikisho ya jamhuri ya Ujerumani chama hiki kikiwa kwa muda mrefu katika nafasi ya tatu na kuchukua ile nafasi ya kuwa chama kinachoamua nani wa kuiongoza Ujerumani katika siasa za nchi hiyo. Chama hiki kinachukuwa mwelekeo wa siasa za mrengo wa kati  kati ya vyama vya CDU na CSU pamoja na wasoshol Demokrat na kuunda serikali ya mseto na vyama vyote.

Lakini chama cha kijani kilipopata umaarufu katika miaka ya 1970 na mapema miaka ya 1980 na kuingia bungeni katika mwaka 1983 kilianza kukipa changamoto chama cha waliberali FDP katika hadhi yake. Uhasama ulikuja kuzidi na kuonekana dhahiri shahiri katika uchaguzi wa mwaka 2013 baada ya kutangazwa na tume kwamba chama cha FDP kimeshindwa kufikia asilimia 5 katika uchaguzi na hivyo hakiwezi kuingia bungeni.Hadi leo chama cha FDP hakiwezi kuisahau sarakasi hiyo.

Isitoshe wanachama wengi wa FDP walishajiondowa katika chama hicho na kujiunga na wanamazingira na vile vile baadhi ya wanamazingira wakajiunga na FDP.kutokana na hilo wengi wanajiuliza je serikali ya mseto kati ya muungano wa chama cha Merkel na FDP pamoja na wanamazingira ni jambo linalowezekani. Wengi wanahisi inawezekana lakini yote haya yatajulikana baada ya Septemba 24.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/Jefferson Chase

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW