1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Narendra Modi ahimiza amani kabla ya ziara ya Ukraine

22 Agosti 2024

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema leo kwamba, hakuna mzozo unaoweza kutatuliwa kwenye uwanja wa vita.

Poland I Waziri Mkuu wa India Narendra Modi anatembelea Poland
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema yuko tayari kusaidia kumaliza vita vya Ukraine.Picha: Sergei Gapon/AFP

Kiongozi huyo amesema nchi yake inaunga mkono mazungumzo na njia ya diplomasia kurejesha amani na utulivu.

Ameyasema hayo mjini Warsaw siku moja kabla ya kufanya ziara ya kihistoria nchini Ukraine iliyokumbwa na vita.

"Migogoro inayoendelea nchini Ukraine na Asia Magharibi inatutia wasiwasi sana. India inaamini kwa dhati kwamba hakuna tatizo linaloweza kutatuliwa katika uwanja wa vita.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akikagua gwaride la heshima na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk.Picha: Pawel Supernak/PAP/picture alliance

Vifo vya watu wasiokuwa ba hatia ni changamoto kubwa kwetu sote. Tunaunga mkono mazungumzo na diplomasia kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu. 

Soma pia: Mambo muhimu yanayojenga ushirikiano kati ya India na Urusi

Kwa hili, India iko tayari kutoa msaada wote unaowezekana na nchi washirika wake."

Modi atakuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa India kufanya ziara nchini Ukraine na wa kwanza katika muda wa miaka 45 kuitembelea Poland, ambayo ni mshirika muhimu wa Kyiv.

Serikali ya India imejiepusha kuikosoa Urusi kwa uvamizi wake nchini Ukraine na badala yake, imezitolea mwito nchi hizo mbili kutatua tofauti zao kupitia njia ya mazungumzo.