1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nasrallah aonya kushambulia Tel Aviv.

Munira Muhammad4 Agosti 2006

Mzozo wa Lebanon umeingia waliokuwemo na wasiokuwemo, Israel leo mchana iliwaua wafanyikazi 40 wa shambani katika mpaka wa Syria.

Sheikh Hassan Nasrallah, Kiongozi wa Hezbollah.
Sheikh Hassan Nasrallah, Kiongozi wa Hezbollah.Picha: AP

Nchini israel makombora ya Hezbollah yaliwauawa watu wawili, huku Umoja wa Mataifa ukihofia kuvunjika kwa harakati zake za utoaji misaada kufuatia msururu wa milipuko nchini Lebanon.

Onyo la kiongozi wa Hezbollah, Sheikh Hassan Nasrallah kuwa Israel ikithubutu kuushambulia mji wa Beirut, wapiganaji wake wataushambulia mji wa Tel Aviv…huenda liliangukia pautupu.

Kwani mji wa Beirut ambao umegeuzwa kuwa uwanja wa kivita kwa wiki tatu sasa, leo uliatthirika zaidi, pale Israel ilipofanya mashambulio makali zaidi…pengine katika jitihada za kujibu hujma za makombora ya Hezbollah yaliyowaua watu 8 jana nchini israel.

Maafisa wa Lebanon waliripoti kuuliwa kwa watu 40, baada ya Israel kuutupia mabomu mji wa Qaa, kaskazini mwa Lebanon, walimokuwepo wakulima waliokuwa wakipakia matunda na mboga karibu na jengo la idara ya forodha ya mpakani mwa Lebanon na Syria.

Na kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita hivi Israel ilishambulia na kulipua madaraja manne yanayouinganisha Beirut na miji mingine…pamoja na Syria.

Msemaji wa jeshi la israel alisema hatua ya kushambulia madaraja hayo ilikuwa kuzima juhudi zozote za Hezbollah kupata silaha kutoka Syria.

Chama cha msalaba mwekundu kiliripoti kuwa watu wanne waliouawa walikuwa ndani ya gari lililokuwa likipita katika daraja mmoja kaskazini mwa Beirut.

Waziri mkuu wa Lebanon Fuad Siniora, alisema mashambulizi ya leo nchini Lebanon yalilenga kuididimiza nchi hiyo katika limbwi la umaskini.

“Ni mashambulio yanayozidi kuwuawa watu wasio na hatia, kuharibu miundo mbinu ya Lebanon na kuiharibu kabisa nchi yetu, mbali na kudidimiza uchumi wetu. Kufikia sasa ni watu 900 wameuawa, 3,000 wamejeruhiwa na idadi hiyo inaongezeka kila siku.“ Alilalama Siniora

Kaskazini mwa Israel, juhudi za Israel kusimamisha makombora yanayotoka kusini mwa Lebanon, bado hazijazaa matunda…kwani Hezbollah walifyatua makombora 100 chini ya saa mbili yaliyowaua watu 2.

Mwanamke mmoja aliuawa katika mji wa Maghar, ilhali mtu wa pili alifariki pale kombora la Katyusha lilipoangukia gari lake nje ya mji wa Kiryat Shmona.

Hezbollah pia iliripoti kuwaua wanajeshi 2 katika vita vikali katika mji wa Markaba.

Umoja wa Mataifa ambao unaongoza juhuzi za kutoa msaada kwa wahanga wa viza hivi nchini Lebanon, sasa wanahofia kukwama kwa usambazaji wa msaada kufuatia msururu wa milipuko ya mabomu nchini Lebanon.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW