NATO, EU wamwalika Biden kujenga upya uhusiano na Marekani
24 Novemba 2020Taarifa kutoka ofisi ya Biden imesema rais huyo mteule amesisitiza umuhimu wa kuufufua uhusiano wa Marekani na Umoja wa Ulaya, baada ya kumpigia simu rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula Von der Leyen. Tofauti na matamshi ya Donald Trump ya kuuita umoja huo adui na kuushutumu kuinyima Marekani biashara, Joe Biden ameelezea matumaini yake kwamba pande hizo mbili zitashirikiana katika changamoto zinazowakabili.
Von der Leyen kwa upande wake ameonekana kufurahishwa na mazungumzo yake na Biden baada ya kuandika hivi katika ukurasa wake wa Twitter kwamba "Nafurahi kuzungumza na rais Mteule Joe Biden, huu ni mwanzo mpya wa ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani. Kufanya kazi pamoja kunaweza kuijenga ajenda ya dunia kuhusu ushirikiano wa kimataifa, mshikamano na maadili ya pamoja.
Ishara njema kwa mahusiano mapya ya Marekani na mataifa ya kigeni
Hii ni ishara nzuri na ya matumaini kwa mataifa mengi ya Ulaya baada ya miaka minne ya mgogoro na mvutano chini ya utawala wa Donald Trump. Mkuu wa Baraza la Ulaya Charles Michel kwa upande wake amesema ni muhimu kujenga muungano imara kati ya Ulaya na Marekani. Ameyasema hayo baada ya kumualika Biden mwaka ujao mjini Brussels pamoja na viongozi wanachama wa mataifa 27 yanayounda umoja huo.
Biden tayari ameshazungumza na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson ambao wote wamemtumia ujumbe wa kumpongeza licha ya Trump kukataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Novemba 3.
Hamasa ya wanadiplomasia wa Ulaya kukutana na Joe Biden
Huku hayo yakiarifiwa wanadiplomasia wa Ulaya wana hamu ya kuona namna Biden atakavyoshughulikia suala la Brexit na hasa msisitizo wake juu ya uhusiano wa Marekani na Umoja wa Ulaya ikilinganishwa na kile kinachoitwa uhusiano maalum na Uingereza. Biden pamoja na waziri mteule wa mambo ya nchi za nje Antony Blinken, wote wameikosoa Brexit na kuonesha wasiwasi wao juu ya athari zake kwa amani na kisiwa kilichogawika cha Ireland.
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amesema anamshukuru Biden kwa kusisitiza kuwa Uingereza ni lazima itekeleze mpango wa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya Brexit uliotiwa saini kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza mwaka uliopita.
Soma zaidi:Joe Biden kuteuwa baraza lake la kwanza la mawaziri
Rais huyo mteule wa Marekani pia ameripotiwa kuzungumza na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, akisisitiza ushirikiano wa Marekani kwa jumuiya hiyo pamoja na kanuni yake ya 5 inayosema kuwa shambulizi kwa mwanachama wa NATO ni shambulizi kwa jumuiya nzima jambo ambalo Trump alikuwa hakubaliani nalo.
Chanzo: AFP